Menu
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.


CHAMA cha Waandishi wa Habari mkoa wa Mbeya(MBPC) kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mwanahabari mwenzetu,Danny Mwakiteleko kilichosababishwa na ajali ya gari jijini Dar es salaam.

Mwenyekiti wa MBPC mkoa wa Mbeya,Christopher Nyenyembe amekielezea kifo hicho kubwa ni pigo kubwa katika tasnia nzima ya habari hasa kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao marehemu enzi za uhai wake.

“Mwakiteleko alikuwa kamusi ya kitaaluma na kisima cha fikra,mfumbuzi na mbunifu wa kazi mbalimbali za kihabari na aliweza kufanya kazi zake na kuibua vipaji vya waandishi wengine,hakika wengi hawatakuja kumsahau”Alisema Nyenyembe.

Kwa kutambua uwezo aliokuwa nao kwa niaba ya waandishi wa habari mkoa wa Mbeya nachukua fursa hii kutoa pole za dhati kwa ndugu na familia yote ya Mwakiteleko bila kuwaacha marafiki zake wa karibu na wafanyakazi wa New Habari alikokuwa akifanya kazi kama Naibu Mhariri Mtendaji.

Kifo cha Mwakiteleko licha ya kuwa pigo kubwa katika tasnia ya habari kwa namna moja au nyingine kimetuachia fumbo kubwa kwa wanaharakati wengine waliokuwa wakitumia kazi zao kupiga vita vitendo vya hujuma,rushwa na ufisadi wa kutisha katika Taifa letu.

Mwakiteleko alikuwa kioo hasa cha jamii katika kutekeleza majukumu yake,alikuwa mpole,mkalimu na mcheshi wakati wote lakini alikuwa makini zaidi katika usimamizi na utendaji wake wa kazi ambao ulimjengea heshima na nidhamu kubwa katika uongozi wake kama Mhariri kila alipokuwepo.

Tunatambua kuwa kifo ndiyo njia pekee ya kumtenganisha binadamu yoyote na ndugu zake,marafiki na jamaa wa karibu waliozoeana na kwa kuwa hayo ndio mapenzi ya MUNGU,tumuache Mungu aitwe Mungu na jina lake lihimidiwe Milele…AMEN.
IMETOLEWA NA
CHRISTOPHER NYENYEMBE
MWENYEKITI
MBEYA PRESS CLUB

Post a Comment

 
Top