Menu
 

AJALI za barabarani zimezidi kutikisa nchi baada ya jana, basi la Kampuni ya Champion kupinduka na kuua watu nane papo hapo Mkoani Dodoma.Kwa mujibu wa mashuhuda, ajali hiyo ilitokea mnamo saa 8:00 mchana, katika kijiji cha Nala wakati basi hilo likitoka Mwanza kuelekea jijini Dar es Salaam na kwamba, majeruhi 53 wamelazwa katika hospitali ya mkoa Dodoma.

Eneo hilo la ajali ni kilomita 15 kutoka Dodoma mjini na Kamanda wa Polisi mkoani hapa Zelothe Stephen amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, lakini akasema, uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali hiyo unaendelea.

Hata hivyo, kamanda Stephen alisema taarifa za awali kutoka kwa mashuhuda zinaeleza chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva ambaye alishindwa kulimudu gari hilo baada ya kukutana na tuta ghafla.

Kwa upande wa mashuhuda hao, walisema chanzo cha ajali hiyo ilikuwa ni mwendo huo kasi na wakati dereva alipokutana na tuta ghafla tairi la mbele la basi hilo lilipasuka na ndipo lilipopoteza mwelekeo.


Taarifa hizo zilifafanua kwamba, baada ya basi hilo kupasuka tairi moja la mbele na kupoteza mwelekeo tairi lake jingine la mbele pia lilipasuka ndipo likapinduka matairi juu bodi chini.

Mwandishi aliyefika muda mfupi baada ya ajali, alishuhudia baadhi ya miili ikitolewa na baadhi ya marehemu walifariki kutokana na kukosa hewa kutokana na basi hilo kuwafunika wakati matairi yakiwa juu.


Katika tukio hilo, juhudi za kutoa miili ya marehemu katika basi hilo pamoja na majeruhi zilifanyika kwa takriban saa tatu tangu kutokea ajali hiyo hadi mnamo saa 11: 35 jioni.

Katika siku za karibuni nchi imeshuhudia ikitikiswa na ajali za barabarani huku Mkoa wa Morogoro ukiwa umeandamwa zaidi kuanzia ile ya wasanii wa kundi la Five Stars, kati ya lori la Mohamed Enterprises (MeTL) na basi la Hood ambayo magari yote yaliteketea kwa moto.
Chanzo:Gazeti Mwananchi. Picha ya Mtandao

Post a Comment

 
Top