Menu
 


Waziri wa Nishati na Madini,William Ngelej
Waandishi wetu
WAKATI Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ikisema uamuzi wake wa kupandisha bei ya mafuta unahusisha hadi yale yaliyokuwa kwenye akiba, waziri mwenye dhamana ya nishati, William Ngeleja amesema bei hiyo haipaswi kugusa mafuta yaliyokuwapo kwa matumizi ya siku 48 kabla.
Mbali ya Ewura kupishana kauli na Waziri Ngeleja, wasomi nao wameponda sababu zilizotolewa na mamlaka hiyo kuhusu ongezeko hilo la bei kwamba imetokana na kuporomoka kwa shilingi na kupanda kwa bei katika soko la dunia, wakiziita ni za kisiasa na zisizo na uhalisia.


Kauli ya Ngeleja Bungeni
Ngeleja akijibu swali la Mbunge Viti Maalumu (Chadema), Susan Kiwanga bungeni jana mjini Dodoma, alisema bei elekezi iliyotangazwa na Ewura juzi, haitatumika kwa mafuta ambayo tayari yalikuwa yametangazwa na mamlaka hiyo kuwa yatatosha kwa siku 48.Kiwanga alitaka kujua kama bei hiyo itatumika kwa yale mafuta ambayo yalielezwa na Ewura kuwa yangetosha kwa siku 48 kabla ya mengine kuagizwa?Waziri Ngeleja alisema bei ya mafuta itabaki ileile ya zamani kabla ya hiyo mpya ambayo ni elekezi na Serikali itasimamia, kuhakikisha hilo linatekelezeka.“Bei itabaki ileile na serikali itasimamia hilo, hivyo mheshimiwa Susan usiwe na wasiwasi kwa hilo.”


Juzi, ikiwa ni siku kumi na moja tu baada ya kutangaza kushusha bei ya mafuta nchini, hatua ambayo ilisababisha mgogoro mkubwa uliotishia uchumi wa nchi, Ewura iliongeza tena bei ya nishati hiyo.
Petroli imepanda kwa Sh100.34 sawa na asilimia 5.51, dizeli kwa Sh120.47 sawa na asilimia 6.30 na mafuta ya taa kwa Sh100.87 sawa na asilimia 5.30 bei ambazo zilielezwa kwamba zilianza kutumika tangu jana.


Alisema bei hizo mpya zimetokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kuendelea kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania, ikilinganishwa na Dola ya Marekani.Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Meneja Biashara wa mamlaka hiyo, Godwin Samwel alisema kupanda kwa bei hizo kunatokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kuendelea kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania, ikilinganishwa na dola ya Marekani.


Wasomi waponda sababu za Ewura
Hata hivyo, sababu hizo zimepingwa na baadhi ya wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huku baadhi wakisema: “Siasa zimeanza kuingizwa katika masuala yanayohitaji utaalamu.”
Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Dk Azaveri Lwaitama alisema inapaswa kutafutwa njia ya kuuza mafuta kwa bei ya chini kwani kwa sasa suala hilo linaingiliwa na masuala ya kisiasa.


Alisema haiingii akilini kuona kwamba wakati hata machungu ya kukosa mafuta hayajaisha masikioni mwa watu, ghafla Ewura inaibuka na kutangaza kupanda kwa bei ya nishati hiyo.
“Serikali imekubali kuwapo kwa soko huria lakini imeshindwa kuingia jikoni na kupika na matokeo yake inaingilia masuala ya kitaalamu, hizi ni siasa tu,” alisema Dk Lwaitama.


Alisema wananchi wanatakiwa kukataa suala hilo la bei elekezi kwa sababu ni la manufaa kwa serikali na wafanyabiashara pekee na haiwasaidii wananchi wa kawaida.Aliitaka Serikali isimamie mafuta kama inavyoshughulikia umeme nchini na siyo kuwaachia wamiliki wa makampuni ambao wanaamua kupanga wenyewe bei.Dk Lwaitama alisema mafuta yanakuja kwa meli na si ndege na kuhoji hifadhi hiyo mpya imeingia lini mpaka bei zinabadilika ghafla na kuumiza wananchi bila sababu?


Mhadhiri mwingine mwandamizi wa chuo hicho, Profesa Mwajabu Possi alisema ni vigumu kumwelewesha mtu wa kawaida kuwa kushuka kwa shilingi ndiyo sababu ya kupanda kwa bei ya mafuta kwa sababu wengi wanajiuliza lakini hawapati jibu.
“Watu wanajiuliza haya mafuta yalikuwapo kabla ya kupanda kwa shilingi kwa nini yauzwe kwa bei ya juu? Nadhani watu waelimishwe zaidi kuhusu kupanda kwa mafuta,” alisema.


Mhadhiri mwingine mwandamizi wa chuo hicho, Dk John Philemon alisema kupanda kwa bei ya mafuta kunaonyesha wazi kuwa kuna mgongano wa maslahi kati ya Ewura na wafanyabiashara wa mafuta.Mhadhiri huyo alisema kushuka kwa shilingi hakuwezi kuathiri kampuni zote za mafuta na kuuza bei moja, kwa sababu zinatoa mafuta katika maeneo tofauti.


“Kuanguka kwa shilingi siyo jambo lililoanza jana au leo asubuhi wangeacha tu soko huria lifanye kazi lenyewe bila kuingiliwa na Ewura,” alisema.
Mhadhiri mwingine mwandamizi wa UDSM, Dk Eugenia Kafanabo alisema kupanda kwa bei ya mafuta nchini ni kuwakomoa wananchi.Dk Kafanabo alisema hali hiyo itaathiri utaratibu na mipangilio mingine ya wananchi kwa sababu, vitu vingi vitapanda bei hususan gharama za usafiri.
“Shilingi haijaanza kushuka na kupanda leo ni suala la kawaida kwa hiyo hii siyo sababu ya msingi iliyotolewa na Ewura,” alisema.


Ewura yatetea zaidi bei mpya
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu alisema bei hiyo kama ilivyo katika kodi, huanza kutumika wakati inatangazwa bila kujali kama wafanyabiashara wa nishati hiyo, wameuza au hawajauza mafuta yaliyopo katika maghala yao.


“Bei huwa tunatangaza kila baada ya wiki mbili, huo ndiyo utaratibu wetu kwa mujibu wa sheria na kanuni zetu, huwa hivyo kutokana na kubadilika kwa bei katika soko la dunia pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani,” alifafanua Masebu.
Alisema kutokana na mabadiliko hayo, wafanyabiashara mara nyingine wanafaidika na wakati mwingine hupata hasara.


Masebu alisema sura ya bei ya mafuta yaliyomo katika maghala ya wafanyabiashara wa mafuta ina sehemu mbili.Alizitaja kwamba ni: “Kwanza, bei mpya inatakiwa imrudishie mtaji aliyewekeza kwenye akiba aliyonayo. Pili, bei inatakiwa imuwezeshe kuwa na mtaji wa kutosha kuagiza shehena nyingine kwa bei itakayokuwepo kwenye soko wakati anaagiza,” alisema Masebu.Alisema iwapo mfanyabiashara hatamudu bei, hataweza kuagiza upya na mzunguko wa biashara utakwama na hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya mafuta katika soko la ndani.


“Kama akiba ya mafuta kwa wafanyabiashara hawa ingekuwa kigezo cha ukokotoaji wa bei ya mafuta, kila wakati tungekuwa tukihakiki kwenye maghala na vituo nchi nzima kabla ya kutangaza mabadiliko ya bei, zoezi ambalo ni gumu na si utaratibu wa biashara ya mafuta,” alisema.
Huku akitoa mfano Masebu alisema: “Katika toleo la bei za mafuta zilizoanza kutumika Juni 8, 2011, bei za mafuta zilishuka kwa asilimia 4.30 kwa petroli, asilimia 4.8 kwa dizeli na asilimia 5.71 kwa mafuta ya taa. Kushuka huko kwa bei za mafuta kulihusisha pia mafuta yaliyokuwa kwenye akiba.”


Total, Oryx na mawakala wa BP
Akizungumzia tetesi kuwa baadhi ya vituo vya Total na Oryx haviuzi mafuta, Masebu alisema Ewura inafanya operesheni ili kujiridhisha na kubaini ukweli wa tetesi hizo na kwamba kabla ya kuchukua uamuzi ni lazima wapate uhakika.Kuhusu BP, MAsebu alisema vituo vinavyouza mafuta kwa rejareja vyenye nembo ya kampuni hiyo havitakiwi kununua mafuta kutoka katika kampuni hiyo kwa kuwa tayari imefungiwa kuuza mafuta kwa miezi mitatu.


“Vituo hivi vinaweza kuendelea kuuza mafuta lakini mafuta hayo wayanunue kutoka kampuni yoyote ile ila si BP…, kama wana mkataba ni baina yao na BP,” alisema Masebu.Alisema Ewura si kama inawaogopa wafanyabiashara wa mafuta nchini na kusisitiza kuwa mvutano ulioibuka mwanzoni mwa mwezi huu baina yake nao haukuwa katika suala la bei, bali ni njia mpya ya ukokotoaji wa bei.


Bei Dar zatofautiana
Wakati wenye kampuni wakianza kutekeleza bei mpya jana, baadhi ya vituo vimeamua kuuza nishati hiyo kwa bei ya juu hasa dizeli na vingine vikiuza chini zaidi ya ile elekezi.Pamoja na vituo vingi kuuza kwa kufuata bei iliyotangazwa juzi ambayo ni Sh2,114 kwa petroli, dizeli Sh2, 031 na mafuta ya taa yaliuzwa kwa Sh2,005.Baadhi ya vituo viliuza petroli kwa Sh2,100, dizeli Sh2,030 na mafuta ya taa Sh2,000. Hata hivyo, katika vituo vingine dizeli ilikuwa Sh2,034.


Imeandaliwa na Boniface Meena, Fidelis Butahe Hussein Issa na Elizabeth Ernest na Timothy Marko

Post a Comment

 
Top