Menu
 

Chama cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Mbeya mjini, kimesema kimejipanga vyema kuhakikisha kinashinda kwa kishindo, chaguzi ndogo za udiwani wa kata za Majengo na Nzovwe, Jijin Mbeya. Kulingana na ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), uchaguzi ndani ya kata hizo, unatarajia kufanyika Oktoba 2, mwaka huu.

Katibu wa CCM wilaya ya Mbeya mjini, Bahati Makalanzi, amesema wagombea ndani ya Chama tayari wameanza kampeni za kujieleza kwa wana-CCM wenzao ili kuomba kuomba ridhaa ya kusimama kwa tiketi ya chama katika kata hizo.

Amewataja wagombea waliojitokeza kuomba ridhaa, ya kukiwakilisha CCM katika kata ya Majengo kuwa ni Dausen Mshilu, Samwel Mwambona, Philimon Mwaisoloka, Joseph Mwambapa, Hassan Mwalukindi na Hassan Mwasembo na kata ya Nzovwe waliojitokeza ni Isaack Sintufya, Lucius Luoga, Kelly Sichone, Genner Mwaijande na Fred Mwakatenya.

Katibu huyo wa CCM wilaya ya Mbeya mjini amesema kuwa Wagombea hao waliojtokeza ili kugombea kwa tiketi ya CCM, watatumia muda wa siku saba kujieleza ambapo Agosti 24, mwaka huu kura za maoni kuwapata wagombea wawili watakaosimama kwa tiketi ya CCM zitapigwa kwa kila kata” alisema Bahati.

Hata hivyo ameeleza kuwa baada ya kura za maoni kukamilika, itafuatiwa na vikao ndani ya chama ambavyo ni kwa ajili ya kuwajadiri wagombea wote waliojitokeza na kisha kutoa mapendekezo kwa kila ngazi kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa.

 Aidha amefafanua kuwa kikao cha Halmashauri ya CCM mkoa, kinatarajiwa kukaa Septemba Mosi mwaka huu ili kufanya uteuzi, ambapo mara baada ya kikao hicho wagombea wa kata hizo kupitia Chama, watakuwa wamejulikana.

Amesema kinachokipa matumaini makubwa CCM kushinda kata hizo ni kuwa kwa kata ya Nzovwe, aliyekuwa diwani kupitia CHADEMA, alijiuzuru na kujiunga na CCM, huku kwa kata ya Majengo,ambayo ilikuwa inashikiliwa na CCM, diwani wake alifariki dunia.

Post a Comment

 
Top