Menu
 

Wakulima wa zao la kahawa katika picha ya pamoja. 
Wito umetolewa kwa mamlaka zinazohusika katika kusimamia fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji kuhakikisha ujenzi unakuwa imara ili kuepuka uharibifu baada ya muda mfupi.

Endapo wito huo ukizingatiwa utatoa mchango mkubwa kuepukana na tatizo la uhaba wa maji kujirudia.

Akizungumza Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kahawa nchini(TaCRI) Bwana Godfrey Makonganya mbele ya mkuu wa mkoa wa Mbeya John Mwakipesile wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya TaCRI na miaka 77 ya utafiti wa kahawa nchini katika maadhimisho yaliyofanyika katika kituo kidogo cha Mbimba wilayani humo.Amesema tatizo la uhaba wa maji limekuwa likiwakabili wakulima wa kahawa wilayani Mbozi, jambo ambalo linakwamisha jitihada za uzalishaji na uandaaji kahawa kufikia ubora unaotakiwa kwenye soko la kimataifa..

Wakati huohuo Mmoja wa wakulima wilayani humo Bwana Nelson Nzunda ameiomba serikali kuangalia upya namna ya usambazaji wa mbolea za ruzuku ikiwa ni pamoja na kuhakikisha zinapatikana kwa wakati muafaka, na kwamba mila na desturi walizozitumia wazee kwa ajili ya kuhifadhi mazingira ili kukabiliana na janga la ukame linaloikabili nchi zinapaswa kurejewa.

Hakuishia hapo amesema kuwa zao la kahawa linahitaji maji mengi na mvua za uhakika ili kuliwezesha kustawi, hivyo kukosekana kwa mvua katika msimu 2010/2011 kumepelekea wakulima kushindwa kupata mavuno mazuri mwaka huu ilihali bei ya zao hilo ni nzuri.

Kwa upande wake Meneja wa kituo cha utafiti wa kahawa kanda ya Nyanda za Juu Kusini Isaac Mushi alibainisha kuwa katika msimu huu mavuno ya kahawa yanatarajia kushuka kutoka tani 12000 hadi kufikia tani 8000 kwa wakulima wa wilaya ya Mbozi na kuwa hali hiyo inatokana na uhaba wa mvua.

Mushi alielezea mafanikio ya taasisi yake kuwa imeweza kufanikiwa kuviunganisha vikundi 144 vya wakulima ambao sasa wanaweza kuzalisha wenyewe miche ya kahawa chotara yenye ukinzani wa magonjwa sugu ya Chulibuni na kutu ya majani ambayo pia yalipelekea wakulima wengi kukata tamaa ya kuzalisha zao hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mbeya John Mwakipesile ameweka msimamo wa mkoa juu ya biashara ya kahawa mbichi kuwa serikali ya mkoa hatakuwa tayari kumvumilia mtu wa namna hiyo na kuwa atawachukulia hatua kali za kisheria kwani
ununuzi wa kahawa mbichi ni kumnyonya mkulima na kumpunguzia kipato chake jambo ambalo aliliita ni unyonyaji wa wazi unaofanywa na wafanyabiashara kwa mkulima.

Post a Comment

 
Top