Menu
 

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumisha na Utawala wa BOT, Amatus Liyumba akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo huku akikabiliwa na shitaka jipya la kukutwa na simu ya mkononi akiwa gerezani. (Picha na Francis Dande).
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumisha na Utawala wa BOT, Amatus Liyumba akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo.
Liumba akirudishwa Rumande.

Na Ripota Wetu.

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu akikabiliwa na kosa la kukutwa na simu ya mkononi gerezani.

Liyumba (63) anatumikia kifungo cha miaka miwili katika gereza la Ukonga, baada ya kupatikana na hatia ya kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya Umma.

Akisomewa shitaka hilo jana mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Elizabeth Kaganda, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Stuart Sanga, alidai kuwa Julai 27, mwaka huu katika gereza la Ukonga, mtuhumiwa alikutwa na simu aina ya Nokia 1280, ya rangi nyeusi yenye namba 0653004662 kinyume cha sheria ya wafungwa namba 86.

Baada ya kusomewa shitaka hilo yalizuka mabishano ya kisheria baina ya upande wa mashitaka na upande wa utetezi, ambapo upande wa utetezi ukiwakilishwa na Majura Magafu alidai kuwa katika hati ya mashitaka sheria namba 86 ya sheria ya wafungwa kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, haionyeshi kwamba upande wa mashitaka unamshitaki mshitakiwa kwa kifungu gani.

“Ili mshitakiwa aweze kujibu kama ana kosa au la inapaswa makosa yawe yanaeleweka kwamba anatuhumiwa chini ya kifungu gani, tunaomba upande wa mashitaka kufanya marekebisho ambayo yanaweza kurekebishwa hata kwa mkono kwamba wanamshitaki katika kifungu gani cha sheria hiyo,” alidai Magafu.

Akipangua hoja hiyo Wakili Kaganda aliiomba Mahakama itambue kuwa mshitakiwa anashitakiwa kwa kosa la kukutwa na kitu kisichoruhusiwa gerezani.

Wakili Magafu alidai kuwa mashitaka hayo yana dosari hivyo upande wa utetezi hauwezi kumruhusu mteja wao kusema ndio au hapana kwa makosa aliyosomewa, hivyo aliiomba Mahakama kuifuta ili upande wa mashitaka ukaifanyie marekebisho hati hiyo.

“Kifungu cha 86 kina sehemu tatu, ya kwanza inatambulisha kukutwa na kitu kinachokatazwa na Magereza lakini haisemi kosa, ya pili na ya tatu inakataza tu lakini pia inatoa kwa Ofisa wa Magereza kuweza kuiharibu hiyo mali,” alidai Magafu.

Akitoa uamuzi wa Mahakama, Hakimu Sanga alikubaliana na upande wa utetezi ambapo aliutaka upande wa mashitaka kuifanyia marekebisho hati hiyo ya mashitaka na kuahirisha shauri hilo kwa muda ili kutoa nafasi kwa upande wa mashitaka kufanya marekebisho.

Baada ya kufanya marekebisho Mahakama ilirudi tena ambapo Wakili Kaganda alidai kuwa kwa mujibu wa amri ya Mahakama ya kuifanyia marekebisho hati ya mashitaka, upande wa mashitaka umefanya hivyo kwa kutumia sheria ya mwenendo wa makosa ya jina namba 234 ( 1) na (2) na kumsomea upya mshitakiwa shitaka lake ambalo alilikana, na kuiomba Mahakama kuwapangia tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo kwa kuwa upelelezi haujakamilika.

Wakili Magafu kwamba kwa kuwa mshitakiwa anatumikia adhabu ya kifungo ambacho anamaliza Septemba 28, mwaka huu, aliiomba Mahakama kumpatia dhamana, ikitokea kwamba ametoka jela aendelee kuwa chini ya dhamana katika kesi hii.

Hakimu Sanga alisema sheria hairuhusu mtu anayetumikia kifungo kupata dhamana, lakini kwa kuwa kesi hii ni mpya Mahakama inaweza kutoa dhamana.

“kwa minajili ya kesi hii, dhamana iko wazi kwa mshitakiwa kwa kusaini hati ya dhamana ya Sh 50,000 na mdhamini mmoja ambaye anafanya kazi katika sehemu inayotambulika,” alisema Hakimu Sanga.

Mshitakiwa alipata dhamana jana hiyo hiyo na kesi iliahirishwa mpaka Septemba 29, mwaka huu itakapotajwa tena.

Mei 24, mwaka 2010 Liyumba alihukumiwa kwenda jela miaka miwili na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na Mei 28 kupitia ya mawakili Majura Magafu na Hudson Ndusyepo, Liyumba alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam akitoa sababu 12 za kupinga hukumu hiyo pamoja na adhabu.

Hata hivyo, Desemba 21, 2010, Mahakama Kuu ilitupilia mbali rufaa yake na kukubaliana na hukumu iliyotolewa Mahakama ya Kisutu.

Post a Comment

 
Top