Menu
 

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Bwana John Livingstone Mwakipesile, amekemea vikali wanasiasa wanaofanya siasa zao kwa kuwashawishi wanachi kutochangia michango ya maendeleo na kudai kuwa hizo ni siasa uchwara.

Karipio hilo alilitoa Septemba 1 kwenye kikao maalumu cha Baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi kilichofanyika mahususi kujadili taarifa ya mkaguzi na mdhibiti wa fedha za serikali.

Alisema kuwaambia watu wasitoe mchango ama kutaka watoe pungufu na kiwango kilichokubalika si kuwapenda wananchi bali ni kuwafanya wazidi kulala na wasiendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ikiwemo malengo ya milenia.

Mwakipesile alisema mchango wa shilingi 10000 si mkubwa kiasi cha kusema kuwa watu wetu ni masikini wasioweza kumudu kiwango hicho bali huku ni kuwafedhehesha kwani kwa mtu wa kawaida ambaye anaweza kufuga kuku wa kienyeji anaweza kumuuza kuku mmoja tu na akapata kiasi hicho cha fedha.

Aliongeza kwa kusema kuwa kuwaambia wananchi wasichange michango ya maendeleo ni kuwataka waendelee kuwa wapumbavu ili uendelee kuwatawala, jambo ambalo alisema serikali haitakuwa tayari kuliacha liendelee na kuwataka madiwani washirikiane na serikali katika kulikomesha.

Akitoa maneno ya shukrani mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Eric Ambakisye alisema kuwa kitendo cha kuhamasisha wananchi kutotoa michango ni dhambi ambayo wanasiasa uchwara wanawatendea wananchi.

Alitoa mfano wale wanaobeza shule za sekondari za kata kwa kuziita yebo yebo kuwa watambue kuwa wapo wasomi wazuri ambao wanatokana na shule hizo na kuwa zimefika hapo zilipo kwa michango ya wananchi hivyo zinastahili kuendelezwa.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, moja ya chama cha Siasa kiliuza sera ya kupunguza kiwango cha michango kwa wananchi kutoka shilingi 10,000 za sasa na kuwa kati ya shilingi 2500 na 5000 jambo ambalo baadhi yao walilifurahia.

Aidha baada ya uchaguzi kukamilika na kwa kuwa chama hicho hakikufanikiwa kushika serikali wateule wake (Madiwani na Wabunge) wameendelea kuwahamasisha wananchi kutoa michango hiyo pungufu jambo ambalo linapingwa vikali na serikali.

Hata hivyo Katibu Mwenezi Jimbo la Mbozi Mashariki, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Osward Mweluka alipoulizwa kwa njia ya simu alikanusha kuhamasisha watu kutotoa michango, bali alisema kinachofanyika ni kuhamasisha wananchi kutambua mahitaji yao ya maendeleo na kuwa wakishabaini hivyo wanaweza kutoa hata zaidi ya kiwango hicho.

Aliongeza kuwa, kigezo kinachotumika sasa ambapo linatekelezwa agizo la mkurugenzi kuchangisha shilingi 10,000, hali hiyo inawapa mwanya watendaji kufuja mali za umma, hivyo wasitumie kauli za watendaji serikalini kama kauli za umma badala yake wamwache naye Mtanzania wa kawaida afanye maamuzi na kushirikishwa kikamilifu kwani mahitaji hayafanani.

Post a Comment

 
Top