Menu
 


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bw. Sethi Kamuhanda ametangaza rasmi nembo ambayo itatumika katika madhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Bw. Kamuhanda ametangaza nembo hiyo leo jijini Dar es Salaam na kusema kuwa wakati nchi yetu ikisherehekea miaka 50 ya Uhuru Serikali kupitia kamati ya kitaifa ya maadhimisho imeandaa nembo rasmi ya maadhimisho hayo.

Pamoja na ubunifu mwingine uliopo katika nembo hiyo, kuna ujumbe pia unaosomeka kuwa TUMETHUBUTU, TUMEWEZA, TUNAZIDI KUSONGA MBELE.

Akieleza maana ya maneno hayo amesema kuwa kuthubutu ni kufanya jambo kwa ujasili na kusema kuwa, kwa ujasili mkubwa nchi Yetu imethubutu kudai uhuru, imethubutu kujenga umoja miongoni mwa wananchi, imethubutu kuwa na muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar na tumethubutu kujiletea maendeleo katika sekta mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Amesema kuwa katika masuala yote tuliyothubu tumeweza kuyafanikisha na ni dhahiri kuwa taifa limeendelea katika sekta mbalimbali na tunazidi kusonga mbele ili kujiletea maendeleo zaidi.

Aidha, amevitaka vyombo vya habari nchini kuhakikisha kuwa vinaitangaza nembo hii ili wananchi waweze kuielewa vizuri. Pia ameyataka makampuni ya watu binafsi kuhakikisha kuwa wanaitumia nembo hii katika maeneo yao na katika machapisho yao mbalimbali.

Wakati huhuo, amezungumzia suala la kufungwa kwa Uwanja wa Taifa baada ya mchezo wa Ngao ya Hisani uliochezwa kati ya Simba na Yanga tarehe 17 Agosti, 2001 kuwa baada mechi ile kulitokea uharibifu wa vifaa ambavyo vilihitaji matengenezo kabla ya matumizi ya Uwanja.

Bw. Kamuhanda ameeleza kuwa wataalam wa viwanja waliishauri Wizara kuwa uwanja ule unatakiwa kutumika si zaidi ya mara mbili kwa wiki kwa kuwa majani yale ni ya asili na yanahitaji kutunzwa.

Amesema kuwa Wizara imeshawasiliana na TFF kwa kuwa ndio wenye jukumu la kupokea maombi kutoka kwa vilabu kwa ajili ya kutumia uwanja ule, ili wanapoletewa maombi hayo wazingatie masharti ya matumizi ya Uwanja huo.

Ameeleza kuwa mechi za Kimataifa pamoja na zile zinazohusisha vilabu na Timu za kimataifa zitaruhusiwa kutumia uwanja huo lakini kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na wataalamu wa viwanja kuhusu matumizi ya uwanja huo.

Post a Comment

 
Top