Menu
 

 Katuni hii inaelezea uhalisia wa adhabu ambazo hutolewa Mashuleni hususani Tanzania.
 Adhabu za aina hii bado zaendelea? namwisho wake ni lini?

Na mwandishi wetu. 
Shule ya sekondari Swilla iliyopo jijini Mbeya imelalamikiwa na wanafunzi wa shule hiyo kwa kuwachapa viboko ovyo na kuwajeruhi bila sababu za msingi.

Baadhi ya wanafunzi hao wamesema shule hiyo ina tabia ya kuwapa wanafunzi adhabu katika vipindi vya masomo bila sababu za msingi ikiwemo kuchapwa viboko zaidi ya ishirini na kuwasababishia maumivu makali kwa kuwajeruhi vibaya.

Pia wamesema pindi wazazi wanapochelewa kulipa ada kupitia akaunti ya shule hiyo wanachapwa viboko ovyo bila ya wazazi kujua na wanatishiwa kupewa adhabu kali pindi watakapowajulisha wazazi wao juu ya vitendo wanavyotendewa.

Mmoja wa wanafunzi hao Ezekiel Kimaro amesema pindi wanapojeruhiwa vibaya na walimu hao hupelekwa katika vituo vya afya kutibiwa na hulazimishwa kusema uongo kuwa wameumia ili kuwalinda walimu hao.

Aidha amesema mnamo mwaka jana mwanafunzi wa kidato cha pili alipoteza maisha shuleni hapo baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kuchapwa viboko na kukataliwa kupewa matibabu na wazazi wake kwa madai ya kutibiwa na uongozi wa shule hiyo hadi mauti yalipomfika mwanafunzi huyo.

Mwanafunzi huyo amesema kwa mwaka huu zaidi ya wanafunzi ishirini wamehama shule hiyo kwa kuhofia usalama wa maisha yao akiwemo mwanafunzi anayejulikana kwa jina la Roi Assay aliyevunjwa kidole katika mkono wake wa kushoto.

Post a Comment

 
Top