Menu
  MAKAMU MKUU WA CHUO KIKUU CHA TEKU PROF. TULI KASIMOTO AKISOMA RISALA


  PROF. METHEW LUHANGA AKISOMA HOTUBA YAKE CHUONI HAPO LEO.
*****
Na, Gordon Kalulunga, Mbeya

Chuo kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU) kinachomilikiwa na Kanisa la Moravian Tanzania kilichopo mkoani Mbeya, kimesema kitawafukuza wanafunzi wote wanaojiita wanaharakati na kuwa chanzo migomo chuoni hapo.

Hayo yalielezwa jana na Makamu mkuu wa chuo hicho Prof. Tuli Kasimoto alipokuwa akitoa hotuba yake mbele ya mgeni rasmi wa mahafali ya Nne ya chuo hicho Prof. Methew Luhanga.

Prof. Kasimoto alisema kuwa wanafunzi wengi wanalitumia vibaya neno harakati ambapo wengi wao wanalitumia neon hilo kama njia ya kuanzisha migogoro vyuoni badala ya kulitumia vema na kuwa jicho la wanyonge.

‘’Chuo chetu hakitawavumilia wanafunzi wote wanaojiita wanaharakati kama vyanzo vya vurugu chuoni kwetu kwasababu wanaharakati ni watu wanaotetea haki za wanyonge lakini wanaojiita harakati vyuoni wanatafuta umaarufu na hawajui kudai haki zao kwa kufuata wahusika bali hubahatisha’’ alisema Prof. Kasimoto.

 Alisema kuwa watu hao wanaojiita wanaharakati hawana sifa ya kuwa wanaharakati bali ni wanaharakati uchwara ambao hivi karibuni wameongoza mgomo na maandamano chuoni hapo kisa hawajapata mikopo wakati mikopo hiyo wanatakiwa wakadai bodi ya mikopo ambao wana mikataba nao.

‘’Tutapambana na wanaharakati hao uchwara na hatutawafumbia macho bali tutawafukuza kwasababu ya kulinda heshima ya chuo chetu’’ alisema Makamu huyo wa chuo cha Teofilo kisanji.

Kwa upande wake mgeni rasmi wa mahafali hayo Prof. Methew Luhanga alisema kuwa changamoto kubwa inayovikabili vyuo vingi hapa nchini ni kutokana na wanafunzi kutokuwa na fedha za kutosha.

‘’Changamoto kubwa ni kutokuwa na fedha za kutosha kwa wanafunzi suala ambalo linachangia kuwepo kwa migogoro na migomo vyuoni tofauti na awali vilipoanzishwa vyuo vikuu hapa nchini’’ alisema Prof. Luhanga.

Alisema kuwa mbali na suala hilo la ukosefu wa fedha kuwa chanzo cha migogoro vyuoni pia ni chanzo cha kuwa na utafiti hafifu katika vyuo vingi nchini.

Wahitimu 812 walitunukiwa Shahada, stashahada na vyeti vya chuo hicho wakiwa wanawake 293 na wanaume 519 ambao vyeti hivyo ni vya Elimu na uchungaji.

Post a Comment

 
Top