Menu
 

Mkuu wa wilaya ya Mbozi Bwana Gilbert Kimolo akipewa maelekezo na mikakati ya kudhibiti moto uliokuwa ukiendelea katika soko la Kisimani mji mdogo wa Tunduma.
*****
Na Ezekiel Kamanga
Moto mkubwa umeteketeza kabisa soko la Kisimani lililopo mji mdogo wa Tunduma wilaya mpya ya Momba mkoani Mbeya, jana na kusababisha hasara kubwa ya mali kuteketea na baadhi ya watu kujeruhiwa.

Zaidi ya wafanyabiashara elfu moja wameathiriwa kiuchumi kutokana na moto huo ulioanza majira ya saa 10 jioni mara umeme ulipo rudi baada ya kukatika na hivyo kusababisha moto kuzuka katikati ya vibanda ndani ya soko.

Juhudi za kuuzima moto huo zilichukua muda kutokana na mji huo wa kibiashara kukosa gari la zima moto, hali iliyolazimu magari ya maji(boza) yanayotumika kujenga barabara kutoka Mji wa Tunduma kwenda mkoani Rukwa kusaidia kudhibiti moto huo na kusaidiwa na magari mawili ya zima moto kutoka wilaya ya Nakonde ya nchini Zambia ambapo nayo yalishindwa kuzima moto huo.

Hata hivyo magari mawili kutoka jijini Mbeya yalifika eneo la tukio majira ya saa moja na robo usiku ili kudhibiti moto huo.

Uhaba wa maji katika mji huo umechangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha shughuli za uzimaji moto huo kwani magari kutoka nchini Zambia yaliishiwa maji mapema.

Mkuu wa wilaya ya Mbozi Bwana Gilbert Kimolo alifika mapema kutoa pole kwa wahanga na kuwaomba kuwa watulivu kutokana na janga kubwa lililowakuta na kwamba serikali inafanya uchunguzi ili kuweza kubaini chanzo hicho cha moto.

Post a Comment

 
Top