Menu
 



 WANANCHI WAKIWA ENEO LA TUNDUMA MPAKANI MWA TANZANIA NA ZAMBIA


 MAKAZI YA WANANCHI WANAOISHI MJINI TUNDUMA KAMA YANAVYOONEKA


Na Gordon Kalulunga.
 Askali wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania katika mpaka wa Tunduma uliopo kati ya Tanzania na Zambia, wamefanikiwa kuzima machafuko yaliyokuwa yameanza kati ya wasafirishaji wa Tanzania na Zambia.

Sakata hilo lilitokea juzi kuanzia majira ya saa 2 asubuhi na kumalizika majira ya saa 9 alasiri ambapo wasafirishaji wa upande wa Tanzania walikuwa wakinyang’anya funguo za magari ya raia wa Zambia waliokuwa wakivuka mpakani hapo kwa kile walichodai kuwa walichoshwa na manyanyaso.

Walisema kuwa raia wa Zambia wamekuwa wakiwapiga wasafirishaji kutoka upande wa Tanzania hasa wanaosafirisha kwa kutumia Bajaji na pikipiki maarufu kama Bodaboda wanapovuka kwenda eneo la Nakonde kupeleka abiria jambo ambalo walilipeleka polisi mara kadhaa lakini walikuwa wakipuuzwa.

Wasafirishaji hao walisema kuwa tabia hiyo ya wasafirishaji wa upande wa Zambia imedumu kwa takribani muda wa miezi miwili sasa hivyo nao waliamua kujichukulia hatua mikononi ili Serikali za pande zote mbili zichukue hatua kudhibiti maonezi wanayotendewa.

Baada ya hali hiyo kuwa tete, Askari wa Jeshi la polisi katika kituo cha polisi kilichopo  Tunduma waliamua kujitokeza na kuwaomba wasafirishaji hao kutoa kero zao na kile kilichosababisha waanze kujichukulia hatua ili kuwadhibiti raia wa Zambia kutoingia na usafiri wao upande wa Tunduma ambapo wasafirishaji hao walitii ombi hilo.

Askari Polisi hao wenye vyeo mbalimbali wakiongozwa na mkuu wa kituo hicho Aly Wendo waliwasihi wasafirishaji hao kuacha kufanya hivyo kwa kile walichodai kuwa malalamiko yao yalikuwa ya Msingi lakini wakawaonya kuwa ni muhimu wakaheshimu sheria za nchi zingine.

‘’Tunawashukuru kwa uelewa wenu na kutoa malalamiko bila kuficha na sisi kwasababu tunajua maana ya ujirani mwema na askari wa upande wa pili wanauelewa mzuri hivyo mimi ninaenda kule upande wa pili kuwaeleza wenzangu kuwa kuna jambo hilo hivyo atakayepigwa kuanzia sasa aje kwangu tunavuka nae na kuwakamata wale watakao husika’’ alisema Wendo.

Kwa upande wake Inspector Chaburuma na askari wengine ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja waliwafafanulia wasafirishaji hao kuwa sheria za nchi ya Zambia hazitambui usafiri wa Bodaboda na bajaji hivyo ni muhimu wakaheshimu suala hilo licha ya kuwepo mazoea ya ujirani mwema.

Kwa upande wao wasafirishaji hao zaidi ya 100 waliokuwa wametoka eneo la mpaka huo walipokuwa wamezingira na kisha kuelekea katika kituo cha polisi baada ya kuombwa na askari polisi wa Tunduma waliwahakikishia askari hao kuwa wamekubaliana na ushauri huo na hasa kutokana na Mkuu huyo wa kituo kuonesha utu wa kufuatilia upande wa pili ili kumalizwa kwa mgogoro unaoweza ukuathiri uchumi wa watu wanaotegemea mpaka huo.

Msafirishaji Hamad Omary alisema kuwa kutokana na kueleweshwa na askari hao msafirishaji yeyote ambaye atakiuka makubaliano hayo wenzake hawatahusika na lolote.

Post a Comment

 
Top