Menu
 MKUU WA MKOA WA MBEYA ABBAS KANDORO
*****
Na mwandishi wetu.
Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imempa kazi nzito ya kutatua migogoro Mkuu wa mkoa Abbas Kandoro na idara ya usalama wa Taifa ikihofia kusutwa na wananchi wakiwemo wananchi wa kijiji cha Isunura, imebainika.

Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa ofisi hiyo imekuwa ikipelekewa malalamiko na wananchi juu ya utendaji mbovu wa viongozi wake lakini haitaki kuchukua hatua zozote mpaka imefikia hatua wananchi kuanza kujichukulia hatua mikononi kudhibiti viongozi wabadhilifu wa mali za umma.

Wakizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, wananchi wa kijiji cha Isunura chini ya baraza la wazee wa kijiji hicho walisema kuwa kwa sasa kijiji chao hakina uongozi wa Serikali ya Kijiji jambo ambalo limesababishwa na ofisi hiyo ya Mkurugenzi wa wilaya ya Mbarali.


Mwenyekiti wa baraza hilo Chifu Victory Mpalile alisema kuwa, kijiji hicho kimekuwa kikiyumbishwa mara kadhaa na ofisi ya Mkurugenzi hali ambayo imekuwa ikizorotesha maendeleo ambapo mpaka sasa zaidi ya miezi kumi hakuna shughuli zozote zinazoendelea kutokana na Serikali kutoweza kutoa maamuzi yaliyo wazi ya kijiji hicho kuwa katika kata ipi kati ya kata ya Igava na Mawindi.


‘’Wialaya hii rushwa imezidi na wananchi wanapodai haki tunaonekana ni wakorofi kwasababu hatukubaliani na mambo yao ya kutuburuza na kutokana na hilo mpaka sasa hatuna uongozi wa Serikali ya kijiji kwasababu hawa waliokuwepo wamevuliwa uongozi kutokana na vitendo vyao vya rushwa’’ alisema Chifu Mpalile.


Alisema Novemba 20, mwaka huu, wananchi wa kijiji hicho baada ya kuiandikia ofisi ya Mkurugenzi barua na mihutasari tangu mwanzoni mwa mwaka huu juu ya malalamiko ya kutokuwa na imani na Ofisa mtendaji na Mwenyekiti wa Kijiji hicho Silivyo Mbishila na kupuuzwa waliamua kuchukua funguo za ofisi na mihuri ya Kijiji hicho chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi.


Sanjari na hayo alimuomba Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro na idara ya usalama wa Taifa kufika kijijini hapo na kuwasikiliza kilio chao ili pia waunde serikali ya muda kwa ajili ya huduma za kijamii za Kijiji hicho.


Kwa upande wake Katibu wa baraza hilo la wazee Vitus Mbishila alisema kuwa kilichowapelekea wananchi hao kuchukua mihuri kwa maandamano kutoka kwa ofisa mtendaji na Mwenyekiti wake ni kutokana na kuwepo mazingira ya kuuza ardhi yao zaidi ya kilomita 3.


Mwenyekiti wa wafugaji wa Kijiji hicho Nicorous Kikwembe alisema kuwa kabla ya suala hilo, baadhi ya wafugaji walikamatwa katika kijiji hicho na kupelekwa mahakamani lakini kutokana na Mwenyekiti huyo kutokuwa mwaminifu alienda kuwa shahidi wa wafugaji hao hatimaye wafugaji wakashinda kesi.


Kwa upande wao Josephine Mdimilage  ambaye ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Luvalanda,  Bibi kizee Ashura Nguluva (90) walisema kuwa eneo hilo lililotaka kuuzwa na viongozi hao lina hati miliki ya mawe na hata wilaya pia wanalijua hilo.


Aidha mbali na hilo waliiomba Serikali kufanya hima kutatua matatizo baina ya hicho na Serikali ya wilaya hiyo kwasababu kutokana na Serikali kukisusa kijiji hicho imefikia wanawake wajawazito kukosa hata huduma za kliniki katika zahanati iliyopo Kijijini hapo ambapo hulazimika kutembea zaidi ya kilomita Nane mpaka eneo la Rujewa.


Juhudi za kumpata Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo George Kagomba ziligonga mwamba baada ya kufika ofisini kwake na kuelezwa na katibu muhtasi wake kuwa alikuwa nje ya ofisi.

Post a Comment

 
Top