Menu
 

Salam,

Baada ya kuzindua album yao ya Kumi na Moja, yenye jina 'Dunia Daraja' kwa kishindo katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam, siku ya Jumapili, tarehe 6 Novemba 2011, Kundi zima la African Stars, wana Twanga Pepeta, Kisima cha Buruduni wameamua kuvinjari viwanja vya kimataifa kwa kutembelea Jiji la London kuja kusugua kisigino na wapenzi wao walioko Uingereza na nchi jirani.

Katika kusherehekea maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania, kundi hilo lililokamilika katika safu zake za waimbaji, wapiga vyombo na wacheza show linatarajiwa kuwasha moto wa burudani yao siku ya Jumamosi, tarehe 26 Novemba 2011 katika Ukumbi wa Club 2000 Savoir Banqueting Suite, Popin Building Southway, Wembley HA9 0HB kuanzia saa Tatu Kamili Usiku mpaka alfajiri (9pm  til late).

Mheshimiwa Balozi Peter Kalaghe atakuwa mgeni rasmi. CD za album mpya na za zamani zitauzwa na vinywaji pamoja na vyakula vya kitanzania vitakuwepo vya kumwaga. Viingilio vitakuwa £20 (singles)  na £30 (couples) kabla ya saa sita (mid night) na £25 (singles) na £40 (couples) baada ya saa sita usiku.

Njoo tujumuike, njoo usugue kisigino, njoo usherehekee uhuru wa nchi yako, njoo ule na kunywa kitanzania. Burudani ni watu na watu ni pamoja na wewe. Tanzania itajengwa na watu wenye moyo kama wewe. Karibuni sana.

Shughuli hii imeandaliwa na Urban Pulse Creative, chini ya maelekezo thabiti ya Ubalozi wa Tanzania, London. 'Tumethubutu, Tumeweza na Tunaendelea Mbele.

Post a Comment

 
Top