Menu
  Dr.MARY MWANJELWA (Kushoto) akipeana mkono na Meneja mfawidhi wa bima ya Afya ya Taifa CELESTIN MUGANGA.
*****
Na Gordon Kalulunga
BIMA ya Afya ya Taifa (NHIF) Kanda ya nyanda za juu kusini imewahamasisha wananchi mkoani Mbeya kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) unaowezesha familia ya watu sita kutibiwa kwa gharama ya Shilingi Elfu kumi kwa mwaka mzima.

Hali hiyo ilijidhihilisha katika uzinduzi wa gari la uhamasishaji wa kujiunga na mfuko huo wa Afya ya jamii uliozinduliwa na Mbunge wa Viti maalum mkoani Mbeya Dr. Mary Mwanjelwa (CCM) katika viwanja vya mikutano vya Ruanda Nzovwe vilivyopo Jijini Mbeya.

Akizungumza katika viwanja hivyo, Meneja mfawidhi wa mfuko wa bima ya Afya (NHIF) Celestin Muganga alisema kuwa mfuko wa Afya ya jamii (CHF) ni tiba ambayo inamwezesha mwananchi kutibiwa kwa kutumia kadi atakayopewa baada ya kujiunga.

Alisema kuwa kwa mkoa wa Mbeya wananchi wengi watajiunga baada ya kupata elimu ambapo wananchi wa wilaya ya Rungwe wamekuwa na mwamko mkubwa na wengi wao wanafaidika na huduma za Afya kupitia mfuko huo.

Kwa upande wake Dr.Mary Mwanjelwa alisema kuwa licha ya mfuko huo kuwa na manufaa kwa wananchi lakini ni muhimu watendaji wa mfuko wa Taifa wa bima ya Afya kutembelesa wagonjwa Hospitalini ili kujua kama huduma wanazozipata zinalingana na matarajio ya mfuko huo na adhima ya Serikali kuwekeza katika mfuko huo.
 
Naye Mwenyekiti wa bodi ya Afya ya Jiji la Mbeya Andalalisye Mwaihabi alisema kuwa wananchi wengi wanajitokeza kujiunga na mfuko huo na kwamba tatizo lipo nje ya mji kutokana na kutofikiwa na wahamasishaji.

Naye Afisa wa bima ya Afya mkoa wa Mbeya Reginald Kileo alisema kuwa faida ya mfuko wa Afya ya jamii ni pamoja na kupata huduma za kutwa na kulazwa katika Hospitali zote ndani ya wilaya husika, vipimo vya maabara, Huduma ya upasuaji kulingana na utaratibu uliowekwa na Halmashauri husika.

Aidha alitanabaisha kuwa ili kujiunga na mfuko huo wananchi watatakiwa kufika katika vituo vya Afya vilivyo karibu na mahali wanapoishi au kuwasiliana na mganga mfawidhi wa kituo, Mganga wa Hospitali ya wilaya, Mratibu wa bima ya Afya au Ofisi ya Kanda ya Mfuko wa Taifa wa bima ya Afya (NHIF).Dr. Mary Mwanjelwa alikabidhi gari la uhamasishaji kwa Mwenyekiti wa bodi ya Afya ya jamii Jiji la Mbeya Andalalisye Mwaihabi aina ya Land Cruser lenye namba za usajili SU 38619.

Wananchi zaidi ya kumi na tano walihamasika na kujiunga na mfuko huo wa Afya ya jamii (CHF) ambapo mmoja wa wananchi  hao John Joshua Muro mkazi wa eneo la Ilomba alisema kuwa alihamasika na kujiunga kutokana na kuona faida za watumishi wa Serikali wanaotibiwa kupitia kadi za bima ya Afya ya Taifa.


Post a Comment

 
Top