Menu
 

Makaburi mawili yafukuliwa  katika kitongoji Matweli, kijiji cha Ibililwe na Ibililo Kata ya Nkunga mkoani Mbeya kwa kile kilichodaiwa kuwa ni imani za kishirikina likiwemo kaburi lililofukuliwa ni pamoja na la marehemu Ndengelapo Masinga (84) ambaye alifariki mwaka 1985 kwa kucharangwa kwa mapanga na watu wasiojulikana.

Siku ya ijumaa, Desemba 9 mwaka huu katika kijiji Ibililwe watu wasiojulikana walifukua kaburi hilo na kuchukua baadhi ya mabaki ya mwili wake uliokuwa umezikwa katika mashamba yake.

Kaburi hilo lilikuwa limejengwa kwa matofali ya kuchomwa  ambapo waliyaondoa na kutoa udongo hadi kuyafikia mabaki ya mwili wa marehemu Masinga.

Aidha inadaiwa kulikuwapo na mvutano baina ya wanandugu wa marehemu Masimba na wananchi baada ya kufukuliwa kwa kaburi hilo na kubaki futi mbili  ambapo wananchi walichukua jukumu la kulifukua licha ya kukuta mabaki ya kipande cha mkeka tu. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji Bwana Jackson Kaposolo, Mwenyekiti wa kitongoji Bwana Kefasi Mwangelo na Afisa Mtendaji wa kijiji Bwana Ephraim Njole waliitisha mkutano wa wanakijiji ambao ulihudhuriwa na machifu.

Haya hivyo habari zisizo rasmi zimeeleza kuwa ni mbinu mpya za waganga wa kienyeji kutaka mabaki ya watu waliofariki kwa ajali au kuuwawa na watu.

Naye Chifu Watson Kakende amelaani vikali tabia hizo ambapo alionekana akitokwa na machozi, kutoa onyo kwamba yeyote aliyehusika na tukio hilo hatofapata mafanikio yoyote endapo atajipatia fedha kupitia mabaki hayo na kudai kuwa atadhurika.

Kaburi la pili katika kijiji cha Ibililo ni la marehemu Kakina Mwampyate ambalo nalo lilifukuliwa siku hiyo hiyo ambapo marehemu huyo alifariki miaka miwili iliyopita ambaye aliuawa kwa kukatwakatwa na mapanga hadi kufa na watu wasiojulikana na mazishi ya mwili huo kufanyika katika shamba lake.

Mtoto wa marehemu Bwana Anosisye Pakima Mwampyate (Kitonga) alishtushwa baada ya kukuta kaburi la baba yake lipo wazi alipoangalia ndani alikuta mabaki ya mwili wa baba yake yakiwa yamechukuliwa na kutoa taarifa katika ofisi ya serikali ya kijiji.  

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho Bwana Emmanuel Mwaisumo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuitisha mkutano na wananchi na  kulaani vikali tabia hiyo na inayohusishwa na imani za kishirikina.

Post a Comment

 
Top