Menu
 

Na Ezekiel Kamanga, Tunduma.
Wimbi la watoto kutumbukia visimani na kufariki dunia limezidi kutanda katika mji wa Tunduma, wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya ambapo mtoto wa kike Anjela Adam Haonga mwenye umri wa miaka mitatu na nusu amefariki dunia baada ya kutumbukia katika kisima cha maji kinachomilikiwa na Edson mkazi  wa Kilimahewa.

Tukio hilo limetokea jana majira ya saa kumi na mbili jioni, mtoto huyo alipotoweka nyumbani na juhudi za kumtafuta kugongwa mwamba hadi alipokutwa saa nne usiku katika kisima hicho akiwa amefariki. 

Baba wa mtoto huyo Bwana Adam Haonga amesema wakati wa tukio hilo hakuwepo nyumbani, na kwamba taarifa za kupotea kwa mtoto huyo zilikuja wakati mama wa mtoto Bi Anna Sichimata akitaka kumuogesha mtoto huyo na kubaini kuwa hayupo eneo la nyumbani alikokuwa akiishi na wazazi wake hao.

Kwa upande diwani wa kata ya Tunduma Bwana Frank Mwakajoka amewataka wa miliki wa visima vya maji kuviweka katika hali ya usalama ili kunusuru vifo vya wananchi. 

 Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika kituo cha afya cha Tunduma huku Jeshi la polisi likiendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.


Post a Comment

 
Top