Menu
 

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya ufundi, Mheshimiwa Philipo Mulugo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Songwe wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.
*****
Na, Gordon Kalulunga, Mbeya.
Naibu Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi nchini Philipo Mulugo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songwe wilayani Chunya mkoani Mbeya, ameendelea kutekeleza ahadi zake kwa kujenga maktaba ya wilaya ya Chunya jimboni humo.

Mulugo ametekeleza ahadi hiyo ikiwa ni miezi miwili kupita baada ya kuzipatia vitabu vya ziada na kiada shule za Sekondari Jimboni humo huku akiwapatia Kompyuta ndogo (LAPTOP) waratibu elimu wakata zilizopo Jimboni humo kwa ajili ya kuendeleza elimu.

Akizindua maktaba hiyo iliyopo eneo la kata ya Mkwajuni juzi, Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro alisema kutokana na watanzania wengi kutokuwa na tabia ya kujisomea, hivyo umefika wakati kubadilika na kuanza kujenga kasumba ya kujisomea machapisho mbalibali kutokana na huduma hiyo kusogezwa vijijini.

Alisema wananchi lazima watambua kuwa wanaposoma vitabu wanazungumza na watu wenye ubongo wa hali ya juu ambao walikaa na kuamua kutunga, hivyo kupitia vitabu hivyo watapata maarifa mapya ambayo yatawasaidia kuinua maisha yao katika sekta kwa mfano ya kilimo, afya, biashara nk.

Alisema  wananchi wa wilaya ya Chunya waitumie maktaba hiyo kujisomea machapisho mbalimbali ambayo ndani yake kuna maarifa ya kisasa, kijamii, kielimu, kiuchumi na teknolojia ambavyo vyote hivyo vitaweza kukabiliana na changamoto zinazowakabili.

Sanjari na hayo alisema kuzinduliwa kwa maktaba katika wilaya hio ni jambo muhimu kwani wilaya 17 pekee ndizo zenye maktaba kati ya wilaya zaidi ya 142 za Tanzania Bara ambapo wilaya ya Chunya tayari imeingia katika historia hiyo ya kuwa na maktaba inayoendeshwa kwa ushirikiano wa kati ya Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania na Halmashauri za wilaya.

Kandoro pia alitumia fursa hiyo kumfagilia Mbunge wa  Songwe wilayani hapa, Phillipo Mulugo kwa jinsi ambavyo amekuwa mstari wa mbele katika kusaidia jimbo lake kuliletea maendeleo hususani katika sekta ya elimu na kwamba wananchi wa wilaya hiyo wamuunge mkono kwa kuhakikisha wanasoma ili waweze kuinua hali zao za maisha.

Alisema Mulugo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, amekuwa akifanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi wake lakini kazi hiyo anayoifanya mfano katika sekta ya elimu lazima aungwe mkono kwani malengo yake makuu ni kuwasaidia wananchi ili waondokane katika hali ya ujinga.

Kwaupande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba nchini Dk.Alli Mcharazo, alisema Mbunge wa Songwe wilaya Chunya, Mulugo ndiyo chanzo cha kuomba kuanzishwa kwa maktaba ya wilaya ya Chunya ambayo baada ya kufunguliwa imeingizwa kwenye mtandao wa maktaba nchini.

Dk.Mcharazo alisema maktaba hiyo imepewa jumla ya vitabu 2034 vya masomo yote na kwamba sasa jukumu limebaki kwa wananchi kuitumia maktaba kujisomea ili waweze kupata maarifa yatakayowasaidia kupata maendeleo ya haraka.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro, alimshukru Mbunge wa Jimbo la Songwe, Philipo Mulugo kwa jinsi alivyopigania hadi kupatikana kwa maktaba hiyo na kamba uongozi wa wilaya utahakikisha unawahamasisha wananchi wajenge utamaduni wa kujisomea.

Akizungumza kwa njia ya simu, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya ufundi ambaye pia ni Mbunge wa jimbo hilo Philipo Mulugo abaye hakuwepo eneo la tukio la ufunguzi wa Maktaba hiyo alisema kuwa ameamua kujikita kwanza katika elimu ambapo alisema atatekeleza ahadi zake zote.

Post a Comment

 
Top