Menu
 

Padri Mbeya atimua walimu
      Walala nje siku mbili
*       DC ashuhudia
******  
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Padri wa Jimbo la Kanisa Katoliki mkoa wa Mbeya amewatimua kazi na kutupa vyombo vyao nje walimu saba waliokuwa wakifundisha shule ya sekondari ya wasichana ya Mtakatifu Fransisko iliyopo Forest jijini hapa baada ya kukataa kutoka katika nyumba za shule hiyo wakisubiri uamuzi wa mahakama.

Tukio hilo lilitokea Desemba 24,  mwaka huu  katika eneo la shule hiyo na kuzusha vurugu ambazo zilizimwa na Mkuu wa wilaya ya Mbeya Evance Balama aliyefika eneo la tukio na kusikiliza pande zote mbili.

Uongozi wa shule hiyo inayomilikiwa na Jimbo katoliki la Mbeya iliiomba kampuni ya Yono Auction Mart and Cout Broker tawi la Mbeya kuwatoa kwa nguvu walimu hao ambao baada ya kuachishwa kazi walifungua kesi katika mahakama ya kazi na kupewa barua na kamisheni ya upatanishi na usuluhishi ya kutoondolewa katika nyumba hizo.

Wakizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio walimu hao walisema kuwa chanzo cha hayo yote bu kuachishwa kazi pasipo kulipwa stahiki zao jambo ambalo lilisababisha kufungua kesi katika mahakama ya kazi.

 Walisema baada ya kufungua kesi lilitokea jaribio la kuwaondoa katika nyumba hizo ambapo Desemba 22 mwaka huu kamisheni ya upatanishi na usuluhishi kupitia mpatanishi Boniface Nyambo ilitoa zuio la kutotolewa katika nyumba hizo lakini agizo hilo likapuuzwa.

Walisema baada ya agizo hilo lenye Kumbukumbu namba CMA/MBY/158/2011 kufika kwa wamiliki wa shule hiyo, walishangaa kupata barua ya kuwaondoa kwa nguvu kupitia kampuni hiyo ya Yono.

Barua hiyo inaeleza kuwa walimu hao walioachishwa kazi walipewa taarifa ya kukabidhi nyumba hizo tangu Octoba 13, mwaka huu kupitia barua yenye kumbukumbu namba

ADV/140/2011 na kwamba kuachishwa kazi kulithibitishwa na CMA Mbeya Octoba 10 mwaka huu.

 ‘’Kutokana na walimu waliotajwa hapo chini kuachishwa kazi na kuthibitishwa na CMA Mbeya tarehe 10.10.2011. Na pia kutokana na uamuzi wa Baraza la Ardhi kuthibitisha kuwaondoa katika nyumba za shule hiyo katika uamuzi wa tarehe 22.12.2011 katika Misceleneous Application No. 7 of 2011. Tunapenda kukujulisha kwamba kampuni yako YONO AUCTION MART AND COURT BROKER imeteuliwa  kufanya kazi ya kuwaondoa kisheria mara moja walimu hao’’ imeeleza moja ya barua hiyo.

Barua hiyo imepelekwa nakala kwa walimu wote waliotajwa ambao ni  Ursula Ndeki, Simon Mapunda, Yesaya Musyani, Benezer Msangi, Leonardina Kagoro, Mary Njele na Ernest Njole.

Baada ya kampuni hiyo kuanza kutekeleza kama ilivyokuwa imepewa jukumu hilo ndipo ukaibuka mzozo kati ya wafanyakazi wa kampuni hiyo ya Yono na walimu hao na familia zao hali iliyopelekea Mkuu wa wilaya ya Mbeya Evance Balama kuingilia kati na kuamuru walimu hao wabaki katika nyumba hizo wakati Serikali ikijaribu kujua ukweli wa sakata hilo.

Msemaji wa shule hiyo Padri Innocent Sanga alikataa kuzungumza na waandishi wa habari juu ya utata huo uliokuwa umejitokeza kwa kile alichosema kuwa ni mapema kuzungumza na waandishi wa habari.

Mwanasheria wa walimu hao Ladslaus Rwekaza alisema kuwa baada ya Padri Sanga kukatalia funguo alilazimika kufungua milango mingine kwa lengo la kuhifadhi mizigo iliyokuwa imetolewa nje na kunyeshewa na mvua siku mbili mfululizo.

Na kwamba anamshangaa Padri huyo kuendesha ibada ya Krismas wakati watu anaowaongoza wakiteseka na order ya mahakama ilikuwa haijafika wakati wa kukata rufaa.

Kamanda wa polsi wa mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi alisema amesikitishwa na tukio hilo na kwamba alimwagiza Mkuu wa polisi wa wilaya kuwafungulia walimu hao lakini mpaka majira ya saa saba usiku walimu hao walikuwa bado hawajafunguliwa milango hiyo na kuwalazimu kuvunja milango.

Mbali na hilo, walimu hao wamelalamikia kuibiwa vitu mbalimbali zikiwemo kamera na kuharibiwa nyaraka mbalimbali za Serikali vikiwemo vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wao na vyeti vya shule.

Post a Comment

 
Top