Menu
 

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Bwana Evans Balama(kushoto) akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya maarufu kama Ndomboro, katika moja ya vikao vya kujadili masuala mbalimbali ya kutatua kero za wakulima .(Picha na Maktaba yetu)
******
Habari na Mwandishi wetu, Mbeya.
Chama cha wafanyabiashara wa masoko jijini Mbeya kimeutaka uongozi wa Halmashauri ya jiji kutowanyanyasa wafanyabiashra hao kutokana na viongozi wa jiji kupandisha ushuru kiholela bila makubaliano baina yao.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa chama hicho Bwana Charles Syonga alipokuwa akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari mkoani Mbeya katika ukumbi wa Chuo cha Wafanyakazi (OTTU), eneo la Kabwe jijini hapa.

Ameyasema hayo kufuatia halmashauri ya jiji kupandisha ushuru kwa wafanyabiashara hao kutoka shilingi 200 hadi shilingi 500 kwa siku kwa wafanyabiashara wanaopanga bidhaa zao mezani, na shilingi kutoka 15,000 hadi shilingi 65,000 kwa mwezi kwa vizimba na nyumba katika masoko ya Uhindini, Sido Mwanjelwa, Soweto, Ikuti, Airport, Mabatini, Isanga, Uyole, Igawilo na Soko matola.

Kufuatia tamko hilo kwa tangazo la halmashauri ya jiji lililotolewa Januari 6 mwaka huu, ambalo limebandikwa maeneo mbalimbali ya jiji na utekelezaji wake kuanza Januari 16 mwaka huu hali iliyoleta mtafaruku katika utekelezaji wake na kisha kusababisha wafanyabiashra wa soko la Ikuti na Soweto kugoma kulipa ushuru huo na kukataa kuingia sokoni kupanga bidhaa zao.

Sakata hilo limepelekea Mkuu wa wilaya ya Mbeya Mheshimiwa Evans Balama kuingilia kati na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Mbeya Bwana Juma Iddi kulitatua tatizo hilo mara moja, agizo alilolitoa Januari 16 mwaka huu.

Baada ya mgomo huo wa wafanyabiashara uliodumu kwa takribani saa tatu baada ya uongozi wa jiji kukubali ushauri wa Mkuu wa wilaya , hali iliyopelekea wafanyabiashara hao kuendelea kulipia ushuru wa awali.

Bwana Syonga wafanyabiashara wengi wao wana mitaji midogo kuanzia shilingi 5,000 hivyo kitendo cha kuwalipisha ushuru wa shilingi 500ni sawa na kudidimiza maisha ya wajasiriamali wa jiji kutokana na uongozi wa jiji kushindwa kuboresha miundombinu ya masoko yote na kushindwa kufanya usafi katika mazingira yanayowazunguka wafanyabiashara hao.

Akienda mbali Bwana Syonga amesema wafanyabiashara waengi wamekuwa wakipata huduma ya choo cha kulipia  kwa gharama ya shilingi 200 na endapo biashara siku hiyo itatetereka , mafanyabiashara anaweza kutumia shilingi 600, hivyo mwisho wa siku kurudi nyumbani akiwa hana kitu.

Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu umebaini kuwa halmashauri ya jiji imekuwa ikikusanya shilingi milioni 260, kwa mwaka kutokana  na ushuru huo wa shilingi 200, pesa ambayo ni nyingi ukilinanisha na huduma anayopewa mfanyabiashara.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Jiji Bwana Juma Iddi hakuwa tayari kuzungumzia lolote, na kwamba atatoa tamko lake leo katika ofisi za halmashauri ya jiji.

Post a Comment

 
Top