Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Watu wawili wamefariki dunia na wanne kujeruhiwa kwa radi katika mji mdogo wa Tunduma, wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya.

Tukio la kwanza limetokea katika kijiji cha Nkangamo ambapo watoto wawili Chipepo Simtenda (16) na Alfa Sinkamanga(15) walipigwa na majira ya saa 10 jioni wakati wakicheza nyumbani kwao na kufariki papo hapo.

Hata hivyo walikimbizwa katika Kituo cha Afya cha Tunduma ambapo Daktari Mussa Mwakalyele alithibitisha vifo vyao na kudai kuwa mshituko ndio uliosababisha vifo hivyo kwani miili yao haikuwa na majeraha yoyote.

Aidha diwani wa kata hiyo Nkangamo mheshimiwa Simweli alipeleka taarifa katika Kituo cha Polisi Tunduma kisha kuruhusiwa kuondoka na miili ya marehemu kwa taratibu za mazishi kijijini hapo.

Wakati huohuo katika kitongoji cha Sogea Tunduma wilayani huo, watu wanne wamenusurika kifo na kisha kukimbizwa katika Kituo cha Afya cha Tunduma ambapo kati yao watu watatu wameruhusiwa kurudi nyumbani na Bi Devotha Mushi anaendelea kupatiwa matibabu.

Kwa upande wake Daktari Mussa Mwakalyele amesema kuwa majeruhi wote ni wakazi wa Sogea Tunduma na kwamba hali ya Bi Devotha Mushi hivi sasa inaendelea vema.

Majeruhi hao walitembelewa na Mwenyekiti wa Haki za binadamu wilaya ya Mbozi Bwana Stephano Simwanza.

Post a Comment

 
Top