Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Hali ya wakazi wa Kijiji cha Kapunga, wilaya ya Mbarali mkoa wa Mbeya imeendelea kuwa tete, baada ya mwekezaji wa mashamba ya Kapunga  rice project kumwaga sumu ya kuua mimea, kwa kutumia ndege.

Mnamo Januari 12 hadi 14, mwekezaji kwa kutumia ndege ya kunyunyizia dawa alimwaga sumu hiyo katika mashamba yake, pia na katika mashamba ya wananchi katika eneo linalofahamika kwa jina la Mpunga mmoja, na kusababisha wakulima zaidi ya 140, wanaomiliki zaidi ya hekari 4,000 ya mimea kuathiriwa na sumu hiyo.

Tukio hilo limethibitishwa na Meneja Mkuu wa shirika la Kapunga Rice Project Bwana Wally Vermaak, ambaye amesema huyo ni mwanzo tu na wataendelea kumwaga sumu hiyo.

Mwekezaji wakati anamwaga sumu hiyo hakutoa tahadhari wala matangazo kwa wakazi wanaozunguka eneo hilo, hali iliyopelekea sumu hiyo kuwaathiri watu waliokuwa mashambani ambapo mpaka sasa afya zao ni tete kutokana miili na miguu yao kuathiriwa na sumu hiyo na kusababisha baadhi yao kushindwa kutembea.

Baadhi ya wananchi walioathiriwa na sumu hiyo wakati ndege ikimwaga mashambani na kushuhudiwa na mwandishi wa mtandao huu ni pamoja na Bwana Gaidon Peter Ngogo (54), Jailo Esau (22), Jackson Mwandemange  (52), Catherina Shipela (50), Edda Ngosha (35), Julius Isega(50), Ramadhan Nyoni (52) ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji hicho na Raphael Moreli (44) ambaye ni Afisa mtendaji wa kijiji hicho.

Hata hivyo Wizara ya Kilimo ilituma Tume ya uchunguzi na utafiti wa udongo na kutoka mikoa ya Arusha na Dar es salaam, ikiwa na wajumbe wafuateao Bwana Geophrey Mwamengo, kutoka Halmashauri ya wilaya ya Mbarali na Kidemi Peter, Julius Emily Paulo Tarimo, E. Macha, Alex Mlowe ( kutoka TPRI - ARUSHA)  na Mkuu wa Polisi wilaya ya Mbarali B. J Chatanda, ambapo walianza kazi Januari 24 mwaka huu, kwa kuchukua sampuli za udongo na mimea kwa ajili ya kufanyia uchunguzi.

Katika kikao hicho mwekezaji aliendelea kudharau na kutamka kuwa ataendelea kumwaga sumu katika mashamba mengine na kwamba maeneo hayo mengine ni mali yake.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Abbas Kandoro amekiri kupokea malalamiko ya wakulima hao na kwamba suala hilo linafanyiwa kazi na Serikali kuu, hivyo wakulima waendelee kuwa na subira mpaka pale serikali itakapotoa tamko.

Naye Mwenyekiti wa kijiji hicho Ramadhan Nyoni, amesema kuwa kijiji chake kimeendelea kupokea vitendo vya unyanyasaji kutoka kwa mwekezaji huyo vikiwemo vya kuua mifugo, kuteka nyara magari ya wanakijiji kama vile gari namba T 994 AJB aina ya Canter mali ya Bwana Osward Mbeyale (39), Janauri 26, mwaka huu na hivyo wananchi wa kijiji hicho kulazimika kutumia nguvu na kulikomboa gari hilo.

Wakati huo huo wanakijiji wameshindwa kufanyashughuli za maendeleo ya kijiji hicho kutokana na mwekezaji huyo kufunga barabara za kutoka na kuingia kijijini hapo, hali inayosababisha kudhoretesha maendeleo na wakati mwingine wanawake wajawazito kujifungulia njiani kabla ya kufika hospitali.

Wananchi hao wameiomba Serikali kulishughulikia suala hilo haraka ili kuwawezesha kufanya shughuli zao maendeleo ya kijiji na yao vile vile kuepukana na manyanyaso hayo.

Post a Comment

 
Top