Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Mchungaji Geofrey Joram wa Kanisa la Restoration Bible Church (RBC) lililopo Inyala jijini Mbeya amekutwa akiwanga katika nyumba ya Bwana Amanyisye Fungo ambaye anaishi jirani na kanisa hilo.

Tukio hilo limetokea majira ya saa kumi na mbili asubuhi Februari 8, mwaka huu Mchungaji huyo akiwa na baadhi ya waumini wake ambao idadi yake haikuweza kufahamika alikutwa ameshika chupa iliyodaiwa kuwa na dawa ya kienyeji nakuinyunyiza katika mlangoni na chumba ambacho analala Bwana Amanyisye.

Licha ya kutenda tukio hilo mchungaji huyo alifumwa na watoto wa Bwana Amanyisye ambao wanafahamika kwa majina la Baraka Amanyisye (18), mwanafunzi wa kidato cha tatu na Eliud Amanyisye (19) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Lupeta ambao walikuwa wakielekea shuleni kwao.

Watoto hao walipomhoji Mchungaji huyo kwanini anatenda tukio hilo, ndipo mtuhumiwa huyo alikuja juu na kupiga kelele hali iliyompelekea baba wa watoto hao Bwana Amanyisye kuamka, ili kujua nini kilichotokea na alipotoka nje aliwakuta waumini na mchungaji huyo akiwa na chupa mkononi, ambapo alichukua jukumu la kumuita balozi wa mtaa huo Bwana Frank Mwambagi.

Balozi huyo wa mtaa Bwana Mwambagi alipomuuliza mtuhumiwa huyo kulikoni mchungaji alishindwa kujibu na kisha balozi huyo aliamua kwenda kwa Mwenyekiti wa mtaa Bwana Nelson Mahena kutoa taarifa na mtendaji wa mtaa Bi Christina Atakwani ambao walienda kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Iyunga jijini Mbeya.

Hata hivyo Mchungaji huyo alikimbia kusikojulikana, ambapo hata kwake hakuweza kupatikana na waumini wake kutawanyika mara baada ya Viongozi wa serikali ya mtaa kwenda kutoa taarifa kwa Jeshi la polisi Kituo cha Iyunga.

Imedaiwa kuwa mtuhumiwa amekuwa akilalamikiwa kutokana na imani hizo za kishirikina kutokana na kuwashika wanawake sehemu za siri na  matiti wakati akiwafanyia maombezi, na taarifa za uchafu huo zilipelekwa katika uongozi wa mtaa na kumuonya zaidi ya mara tatu lakini alikaidi na kikao cha mwisho cha onyo kilifanyika Februari 2, mwaka huu mbele ya Askofu wake Mkuu Emmanuel Tumwidike, ambapo mchungaji huyo alikiri na kuahidi kumwamisha kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni kukiuka maadili ya kanisa hilo.

Wakati huohuo wakati Askofu Tumwidike akifanya  jitihada za kumuhamisha zikifanyika ndipo mchungaji huyo alipokutwa na tukio hilo na kwamba atalishughulikia leo lakini Uongozi wa Serikali katika mtaa huo uchukue hatua za kisheria.

Mbali na hilo mchungaji huyo anadaiwa kufanya maombi ya kuwaombea wananchi wa mtaa wa Inyala wapate ajali na kufariki kutokana na wananchi hao kumshtumu mchungaji huyo kutokana  na tabia yake mbaya.

Mpaka habari hii inaandikwa mchungaji huyo hajaweza kupatikana licha ya wananchi kufanya msako mkali.

Post a Comment

 
Top