Menu
 

Habari na Angelica Sullusi, Mbeya.
Wakazi wa Kijiji cha Nsambya, Kata ya Iwindi, Wilaya ya Mbeya waliokubwa na maafa kwa kupoteza mazao yao baada ya kuharibiwa na mvua kubwa ya mawe iliyonyesha mwanzoni mwa mwezi februari mwaka huu, hatimaye wamepatiwa msaada.

Msaada huo wenye thamani zaidi ya shilingi milioni 6.8 umetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Evans Balama kijijini hapo akiongozana na Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mch.Lackson Mwanjali,pamoja na Mkurugenzi wa wilaya hiyo Juiana Malange.

Akitoa mchanganuo wa msaada huo Balama amesema kuwa  Halmashauri ya Wilaya  imenunua mbegu ya maharage mifuko 28 yenye kilo 100 kila mmoja na kilo 40 za ziada ambazo zinafanya jumla ya kilo 2,840 yenye thamani ya shilingi milioni 5.9.

Balama amesema kuwa Mbunge wa jimbo hilo kupitia mfuko wa jimbo amechangia shilingi milioni moja ambayo imetumika kununulia mifuko 13 ya mbolea ya kupandia aina ya DAP yenye uzito wa kilo 50 kila moja.

Aidha,Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wakazi hao walioathirika ambao ni kaya zipatazo 71 kugawana msaada huo wa mbegu kwa uwiano sawa wa kila mmoja kupata kilo 40 za mbegu na kilo tisa za mbolea.

Mapema Februari 5,mwaka huu Kijiji cha Nsambya kilikubwa na maafa yaliyosababishwa  na mvua kubwa iliyoambatana na mawe, iliyonyesha kwa zaidi ya masaa 12 bila kukoma hivyo kuharibu mazao ya wakulima ekali zipatazo 248 ambapo kaya 71 zimeathirika.

Post a Comment

 
Top