Menu
 


Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mtu mmoja aitwaye Gesho Brown(37), mkazi wa Kitongoji cha Pipe Line mji mdogo wa Mbalizi wilaya ya Mbeya vijijini Mkoani Mbeya amejinyonga chumbani kwake kwa kutumia kamba.

Mwili wa marehemu Gesho ambaye pia amewahi kuichezea timu ya Tanzania Prisons ya jijini Mbeya, uligunduliwa na shemeji yake aitwaye Bahati majira ya saa 5 kamili asubuhi na kutoa taarifa kwa mjumbe wa eneo hilo aitwaye Bi Edda Yusto ambaye naye alitoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa.

Mara baada ya taarifa kumfikia Mwenyekiti wa mtaa huo Bwana Asifiwe Mwakalonge alitoa taarifa katika kituo cha Polisi Mbalizi ambao walifika na kuuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika Hospitali ya Ifisi kwa uchunguzi.

Hata hivyo sababu za kifo chake hazijabainishwa na marehemu alikuwa akiishi pekee yake nyumbani.

Wakati huo huo wananchi wa kijiji cha Sheyo kata ya Ibaba wilaya ya Ileje wamemwachisha uongozi Mwenyekiti wa kijiji hicho Bwana Denison Simbeye pamoja na serikali yake baada ya tuhuma za wizi wa ng’ombe wa kijiji wenye thamani zaidi ya shilingi laki tatu za kitanzania.

Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano wa hadhara ulioanza majira ya saa nne asubuhi na kumalizika saa 11 jioni ambapo mkutano uliazimiwa na mwenyekiti huyo na serikali yake wachukuliwe hatua za kisheria.

Katika mkutano huo wananchi waliwasimika Bwana Reuben Shibanda na wenzake kuchukua nafasi zilizoachwa wazi na viongozi waliondolewa kutokana na ubadhilifu.

Post a Comment

 
Top