Menu
 


Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mtu mmoja amefariki dunia, baada ya kugongwa na gari katika ajali ya barabarani iliyotokea eneo la Songwe wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya.

Tukio hilo limetokea Februari 14 mwaka huu majira ya saa 12:30 ambapo gari aina ya Scania yenye nambari za usajili T 115 BGR, linalomilikiwa na kampuni ya mabasi ya Ilasi, lililokuwa likiendeshwa na dereva Brown Msaka (44) mkazi wa Dar es salaam ilimgonga mtembea kwa miguu Seth Laiton Mwalinda (28), mazai wa Songwe na kumsababishia kifo papo hapo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa Advocate Nyombi, amethibitisha kutokea kwa tukio hili na kwamba chanzo cha ajali hiyo kimetanjwa kuwa ni mwendokasi wa basi hilo.

Aidha amesema kuwa Jeshi la Polisi linamshikilia Bwana Vasco Lwenje (28), kwa tuhuma za kumuua John Ndelwa (27), mkazi wa Chemchemi Februari 14 mwaka huu majira ya saa nne usiku.

Mtuhumiwa ni mkazi wa Kijiji cha Songwe na alikutwa na simu ya marehemu baada ya Askari Polisi kuweka mtego na mtuhumiwa kubainika Bwana Vasco ambaye amekiri kuhusika na kifo cha marehemu John, na kwamba simu hiyo ni mali ya marehemu.

Wakati huo huo mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa iliyopo jijini Mbeya na upelelezi zaidi wa tukio hili unaendelea .

Post a Comment

 
Top