Menu
 


Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Poland Shobi anayekadiliwa kuwa na umri wa miaka 45 hadi 50, ameuawa kikatili na watu wasiofahamika kwa kupigwa na vitu butu kichwani na kumsababishia kuvuja damu nyingi katika mtaa wa Pambogo Isengo kata ya Iyela jijini Mbeya.

Tukio hilo limetokea katika Uwanja wa ndege jijini hapa na kukutwa vitambulisho vya marehemu  pembeni ya mwili wake.

Kwa mujibu wa ndugu wa karibu amesema Machi 3, mwaka huu majira ya saa mbili usiku marehemu alidai amepigiwa simu kuwa kuna rafiki yake anatoka nchi ya  Pakistan kupitia Namanga na atakuja moja kwa moja jijini Mbeya kwa basi la Kampuni ya Hood kwa hiyo ampokee Kituo cha mabasi cha Soweto.

Ilipofika majira ya saa 3 usiku marehemu aliaga familia yake kuwa ana kwenda kumpokea rafiki yake kwa hiyo wafunge milango, ndipo watoto wake walifanya hivyo na baada ya kuona muda unazidi kwenda walimtafuta marehemu kwa njia ya simu yake ya mkononi haikupatikana wakati huo mke wa marehemu ambaye ni muuguzi alikuwa kazini  Hospitali ya Rufaa aliyopo jijini hapa.

Hata hivyo watoto walipoona muda unazidi kwenda waliamua kutoa taarifa kwa Balozi Ezelina Mahenge, na asubuhi ilipofika walishtushwa  walipomkuta baba yao ameuawa na kisha kumpigia simu mama yao baada ya kuutambua mwili wa marehemu kuwa ni baba yao.

Jeshi la Polisi mkoani hapa lilifika kuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa uchunguzi  na hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Advocate Nyombi.

Post a Comment

 
Top