Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Wakati ulimwengu ukiwa katika hatua ya sayansi na teknolojia huku jamii ikiwaamini walimu kuwa ni moja kati ya wanataaluma wanaoweza kuelimisha umma kuwa hakuna masuala ya kishirikina lakini Jijini Mbeya si hivyo, Mwalimu kapigwa akihusishwa na masuala ya ushirikina.

Hali hiyo imetokea Februari 6, mwaka huu katika shule ya Msingi Juhudi Ilemi Jijini hapa baada ya wananchi na baadhi ya walimu kumtuhumu Mwalimu Eliud Kyando, kuwa amekithiri kwa kuwa kinara wa kupaka kinyesi cha binadamu katika samani za Mwalimu Mkuu na vyombo vya kupikia chakula cha walimu wa shule hiyo.

Sakata hilo la aibu, baada ya kuvumiliwa kwa muda mrefu hatimaye viongozi wa mila walibaini kuwa aliyekuwa akifanya hivyo ni Mwalimu Kyando ambaye alikuwa akiona wivu kuwa kwanini alikuwa hateuliwi kushika nafasi ya ukuu wa shule hiyo wakati amekaa muda mrefu shuleni hapo na hatimaye ukaitishwa mkutano wa hadhara.

Ulipoitishwa mkutano wa hadhara wananchi walionya kwa mhusika kutoridia vitendo hivyo kuwa visijirudie lakini baada ya wiki mbili, vitendo hivyo vilijirudia na kuonekana kinyesi katika samani za ofisi ya mwalimu mkuu, ofisi za walimu huku milango ikiwa imefungwa!

Baada ya kuona hivyo wananchi waliamua kuitisha tena mkutano wa hadhara na kwenda kumuona Afisa elimu wa Jiji la Mbeya na Mkurugenzi ambapo majibu yake yalikuwa ni kuifunga shule hiyo mara moja na baada ya kuona hivyo wazazi walikasirishwa kufungwa shule hiyo wakati anayedaiwa kuwa ni mhusika, na hapo ndipo vijana wakaamua kumsaka na hatimaye walipomkamata wakamwadhibu mpaka pale alipookolewa na askari Nguguri wa Jeshi la Polisi.
 
Hata hivyo wananchi hawakuishia hapo waliifuata familia ya Mwalimu huyo na kuamuru iondoke ambapo familia ilitii na kuondoka ambapo shule imeamuliwa kufunguliwa, lakini taarifa za uhakika zimeeleza kuwa tukio hilo kwa mwalimu huyo ni la pili ambapo awali alifukuzwa shule ya Msingi Itagano kwa tuhuma hizo hizo za ushirikina.

Wakati huohuo walimu wa shule hiyo walitumia muda wa siku nzima kujadili kitendo cha kupingwa mwalimu mwenzao na kuweka mikakati ya vitendo hivyo visitokee tena, kwani hata mahudhurio ya  wanafunzi hayakuwa mazuri darasani wakihofia vitendo vya kishirikina.

Tukio hili la kishirikina ni la pili kutokea shuleni hapo, ambapo miaka mitano iliyopita mama mmoja aliyekuwa akifanya biashara ya maandazi shuleni hapo, alituhumiwa kujihusisha na imani za kishirikina katika biashara yake na ndipo wananchi wakachukua jukumu la kumfukuza eneo hilo.Post a Comment

 
Top