Menu
 

Huenda kwa wengi, Ngome Yesu ni jengo tu la kufurahisha macho, na kwa wengine ni jumba la zamani tu. Lakini, kuna mengi ambayo yamefichika ndani zaidi ya anavyoliona mtu kwa nje.
Ngome Yesu inapatikana katika Mwambao Wa Pwani, Jiji la Mombasa,Kenya na katika barabara ya Nkrumah, Mtaa wa ‘Old Town’. Historia yake ilianza pale Baharia anayejulikana kama Vasco Da Gama kutoka Ureno alipotua Mombasa mwaka Elfu moja, mia nne tisini na nane. Azma ya safari yake ilikua kutafuta njia za biashara kupitia Bahari Hindi. Kama inavyoeleweka, watu kutoka mataifa tofauti walilipenda sana Bara Africa kwa wingi wake wa malighafi.
Licha ya kuwa Vasco Da Gama na Wareno wenzake  walitaka kufanya biashara na watu wa Pwani, lengo lingine lilikuwa kueneza Dini ya Kikristo. Hili halikuwafurahisha watu wa Pwani, hasa wa Mombasa ambao tayari walikuwa wa dini ya Kiislamu. Kisha, Waarabu wa Oman walitaka kuwatoza Wareno ushuru, jambo ambalo lilizua vita vikali.
Ngome Yesu ilijengwa mwaka 1593 baada ya Mfalme wa Ureno kuamrisha Ujenzi wake. Jengo lenyewe lilijengwa juu ya Jabali na kutumiwa kuilinda Bandari, kama Ngome ya Jeshi kati ya mwaka 1837 hadi 1895 na hatimaye  kugeuzwa kuwa jela ya wafungwa tarehe Moja Julai mwaka 1895.
Mbali na historia yake, uhusiano kati ya Kenya na nchi zingine umeletwa na kuwepo kwa  Ngome hii. Kando na hilo, uhusiano wa kihistoria umekuwepo kati ya Kenya na Ureno kwa sababu yanaashiria kuwepo kwa wananchi wa taifa hilo katika nchi hii. Aliyeichora ramani ya Ujenzi ya Ngome Yesu alikuwa kutoka Italia, hivyo basi uhusiano kati ya nchi yake na Kenya umekuwepo hai tangu jadi pia.
Kwa watu wa Pwani,  Kuwepo kwa jumba hili kunaonyesha uwezo wao wa kupigania uhuru. Lugha ya Kiswahili nayo imebeba maneno kadhaa yaliyotolewa moja kwa moja kutoka katika lugha ya Kireno. “Jemedari” linalomaanisha mkuu wa Jeshi, “Mvinyo” lililo na maana ya Pombe na “Bendera” ni kati ya maneno hayo. Hivyo basi, Ngome Yesu ina umuhimu mkubwa katika Historia ya Pwani na Africa Mashariki kwa jumla.
Jamii ya Pwani imenufaika pia, kwani watu wengi wameajiriwa kama viongozi wa ziara na hata wakuu katika sekta ya Utalii kwa jumla. Biashara kadha wa kadha zinazowanufaisha watu wa Pwani na zinazopendwa sana na watalii wanaozuru Jiji la Mombasa zimefunguliwa. Upishi ni miongoni mwa biashara zinazowavutia watalii kila wanapofika Mombasa.
Mapishi ya vyakula kama Muhogo Wa Nazi, Samaki Wa Kupaka, Samaki wa Chuku Chuku, Mkate Wa Mofa na Pilau ni kati ya vyakula vinavyopendwa sana na Watalii, kwani ni nadra kuvipata katika mataifa yao.
Kampuni za kusafirisha watalii nazo zimefunguliwa kwa sababu ya kuwepo kwa Ngome yesu na Makavazi yake, bila kusahau kujengwa kwa barabara, kuwepo kwa nguvu za umeme, kuboreka kwa usalama na maendeleo ya eneo la Jiji la Mombasa. Kwa kifupi, kumekuwa na maendeleo katika mji wa Mombasa kwa kuwa wanaozuru makavazi haya hutozwa kiingilio na kutoa fedha za kigeni.
Licha ya kuwa Ngome Yesu imeleta maendeleo ya kufurahisha kila anayeifahamu kwa undani, imekuwa ikikumbwa na changamoto kadhaa. Kuta za jumba hili zimekuwa zikiota kutu na kubomoka kwa sababu liko katika ngazi ya bahari, na ni la zamani sana. Fedha zinazotumiwa kwa ukarabati huwa za kiwango kikubwa mno.
Kadhalika, kuwepo kwa michezo ya kuigiza na vitabu vinavyoeleza kuhusu Ngome Yesu na Makavazi yake, pamoja na umuhimu wake kwa undani katika siku zijazo ni jambo linalotazamiwa sana. Vilevile, kuna mtazamo wa kuweza kuitangaza Ngome Yesu na kueleza watu zaidi kuyahusu kwa kutumia vyombo vya habari.
Hatimaye, katika Ngome Yesu, Makavazi yake na Jiji la Mombasa kwa jumla, kuna mengi zaidi ambayo yanapendeza na kuelimisha. Litembelee Jiji la Mombasa ujionee zaidi.
 Picha: jiji la Mombasa,Mtaa wa Old town,NGOME YESU(fort Jesus), Pilau, Samaki wa Kupaka, Samaki wa Chuku Chuku, Muhogo wa nazi..mmh..umependa sio?? tegea, utapata zaidi!!!!!!! 

Post a Comment

 
Top