Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Walimu wanaofundisha katika Shule ya msingi Juhudi Ilemi, Kata ya Iganzo jijini Mbeya wameendelea kupata adha ya vinyesi vya ajabu vya binadamu, ambapo Machi 15 mwaka huu majira ya asubuhi viti vyote vinavyokaliwa na walimu vilikutwa vimepakazwa vinyesi na harufu kali kutanda Ofisi hiyo ya walimu.

Mbali na hili pia mapazia yakiwa yamechomwa na moto wa ajabu unaohusishwa na imani za kishirikina, kwani milango ya ofisi hiyo ilifungwa kwa kufuri na nje akiwepo mlinzi.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bwana Charles Mveya amesema tukio hilo ni mfulululizo wa matukio 17 yaliyofanyika mapema mwaka huu tangu likizo ilipoisha na shule kufunguliwa Januari mwaka huu.

Hali hiyo ilipelekea wazazi kuamua kuitisha mkutano huyo ili kujadili mstakabali mzima wa jambo hilo kwa kuhusisha Afisa Elimu wa Jiji la Mbeya, Wachungaji na wazazi, ambapo vitendo hivyo vilikoma kwa muda wa wiki moja tangu ulipoisha mkutano.

Hata hivyo mkutano uliofanywa hivi karibuni ulimtuhumu Mwalimu Kyando, kuwa ndiye mhusika wa matukio haya kwa lengo la kupata wadhifa wa Mwalimu Mkuu.

Mkutano huo haukumalizika vema kwani baadhi ya wazazi na wananchi walimsakama mwalimu huyo na baada ya kumpata walimpiga na kuokolewa na Jeshi la Polisi, ingawa wananchi walifanya uharibifu mkubwa nyumbani kwake naye kulazwa katika Hospitali ya Rufaa iliyopo jijini hapa.

Ofisi ya Elimu jiji iliingilia kati baada ya kumhamishwa Mwalimu Kyando katika shule hiyo na hivi sasa anaishi mafichoni akiwa na familia yake baada ya kutoka hospitalini.

Aidha Afisa Elimu wa Mkoa Bwana Juma Kaponda, amelazimika kufika shuleni hapo na kujionea hali halisi na adha kubwa kwa walimu wake huku wazazi wasijue kinachoendelea shuleni hapo.

Naye, Katibu wa Muungano wa Jamii Tanzania (MUJATA) alifika shuleni hapo na kuahidi kuwa asasi yake itabidi iingilie kati, ili kukomesha vitendo hivyo baada ya Mashehe na wachungaji kushindwa.

Mbali na matukio hayo shule hiyo ni miongoni mwa shule zinazoongoza kwa kufaulisha wanafunzi kimkoa na kitaifa kwa hiyo matukio hayo yanaweza kuharibu morali ya walimu  na wanafunzi alibainisha mmoja wa walimu wa shule hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbeya Bwana Evans Balama, inaendelea na uchunguzi wa tukio hili ili wanafunzi wasiathirike kimasomo na kuwatoa hofu walimu na kuendelea kufundisha huku serikali ikiliangalia kwa kina jambo hili.

Post a Comment

 
Top