Menu
 


 Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mkazi mmoja wa Mama John Jijini Mbeya aliyefahamika kwa jina la Yona Alimwene (39), ameuawa kwa kunyongwa na mtu au watu wasiofahamika kisha mwili wake kuokotwa umbali wa mita mbili kutoka nyumbani kwake.

Mwili wa marehemu umepatikana majira ya saa nne usiku Aprili 8 mwaka huu ukiwa umeokotwa na wasamaria wema, baada ya kuukuta umetupwa pembeni ya Kituo cha Mafuta cha Mama John (ORYX zamani AMINA’S PETROL STATION).

Wasamaria hao walitoa taarifa kituo cha Polisi na Askari walipofika waliufanyia uchunguzi mwili wa marehemu na kuukuta ukiwa na simu ya mkononi na pesa taslimu shilingi elfu sita vyote vikiwa mfukoni mwa suruali ya marehemu.

Kwa mara ya mwisho marehemu aliwasiliana na mkewe aitwaye Nuru Yona (31) akimtaka mkewe huyo amuandalie chakula, wakati huo marehemu alikuwa akitokea kwa dada yake anayeishi mtaa wa Block T katika kikao cha pamoja cha harusi.

Kabla ya kwenda kwenye kikao cha harusi marehemu Yona alikuwa amefungua duka linalouza vipuri vya magari eneo la Soweto, alikokuwa akifanyakazi katika duka hilo maarufu kama FADIGA USED SPARES.

Mkewe alipigiwa simu na Polisi majira ya saa nne usiku wakimtaka aje katika kituo cha mafuta cha ORYX na kumwambia kuwa mumewe amezirai kitu ambacho kilimshangaza na kuanza licha ya kufichwa kwani mumewe kauawa, ndipo mke wa marehemua alimpigia simu kaka wa marehemu aitwaye Bwana Sanya Alimwene majira ya saa tano usiku.

Aidha kaka wa marehemu Bwana Sanya alitoa taarifa kwa Balozi wa mtaa Bwana Amon Mwaisela, ambapo waliuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Rufaa iliyopo jijini Mbeya.
Baadhi ya walinzi waliokuwa karibu na eneo la tukio wamesema waliona gari ndogo aina ya Tax, na kuutupa mwili wa marehemu kisha kuondoka ambapo walienda kutizama na kumkuta marehemu ameuawa na kutoa taarifa kwa Polisi na kugundua shingo yake imenyongwa.

Hata hivyo Jeshi la Polisi limeendelea na uchunguzi kwa kuchukua sampuli za sehemu ya mwili wa marehemu na kutuma Jijini Dar es Salaam kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuufanyia uchunguzi zaidi, na mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo.

Marehemu ameaacha mjane na watoto wawili, baada ya uchunguzi mwili wake umezikwa kwenye makaburi ya Iyela jijini hapa Aprili 9 mwaka huu na kuacha wakazi wa Mama John katika lindi la mawazo.

Post a Comment

 
Top