Menu
 

Habari na Angelica Sullusi, Mbeya.
Halmashauri ya Jiji la Mbeya limepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 58 fedha ambazo ilikuwa ikizikusanya kama ushuru katika sokoni la Mwanjelwa  lililopo eneo la Sido Jijini hapa kutokana na ajali moto iliyotokea mwezi Septemba mwaka jana. 

Hayo yamesemwa jana na Mweka hazina wa Halmashauri ya Jiji, James Jorojiki wakati akiwasilisha bajeti ya halmashauri ya Jiji hilo mbele ya kikao cha baraza la Madiwani kilichoketi kujadili bajeti ya Hamlashauri kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha.

Jiorojiki amesema kuwa kabla ya kuungua kwa soko hilo, Halmashauri ilikuwa ikikusanya shilingi 270,000 kwa siku kama ushuru kutoka kwa wafanyabiashara, fedha ambazo haikuweza kuzipata tena baada ya soko hilo kuungua.

Amesema kufuatia kupotea ghafla kwa chanzo hicho cha mapato, bajeti ya halmashauri iliathirika na kusababisha baadhi ya miradi iliyokuwa imepangwa kutekelezwa kwenye mwaka huu wa fedha kutofanyiwa kazi kutokana na ukosefu wa fedha. 

Ametaja sababu nyingine ya kuzorota kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni kushindwa kukamilika kwa soko jipya linalojengwa eneo la Mwanjelwa ambalo linatarajiwa kuiingizia halmashauri zaidi ya shilingi milioni 300 kwa siku.

Amesema kuwa wakati wa uandaaji wa bajeti ya mwaka wa fedha wa mwaka 2011/2012 iliaminika kuwa soko hilo litakuwa limekamilika na hivyo mapato yanayotarajiwa kukusanywa sokoni hapo yakaingizwa kwenye makadirio ya bajeti ya mwaka huo.

Jiorojiki asema kuwa kutokana na soko hilo kushindwa kukamilika kwa wakati pia kumechangia bajeti ya halmashauri kuyumba kiasi cha kushindwa kukamilisha miradi mbalimbali kama vile ujenzi wa barabara, shule za msingi na sekondari na miradi ya maji pembezoni mwa jiji ambayo ilipangwa kutekelezwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha.

Post a Comment

 
Top