Menu
 

saif al-islam

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC hivi punde itaondoa madai yake kuwa kesi ya Saif al-Islam Gaddafi ihamishiwe The Hague, maafisa wameiambia BBC. Wamesema kesi ya mtoto huyo maarufu zaidi wa kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi badala yake inaweza kusikilizwa ndani ya Libya lakini kwa usimamizi wa ICC. 
 
 Suala la kuwa nani ataiendesha kesi yake limekuwa likizungumzwa tangu alipokamatwa mwezi Novemba mwaka jana. Mahakama ya ICC inamshtaki kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu. Kwa sasa wizara wa Sheria ya Libya inasema makubaliano yanakamilishwa ambapo Bw Gaddafi anaweza kuhukumiwa nchini Libya lakini kukiwa na ulinzi na usimamizi wa Mahakama ya Kimataifa. 
 
Mwandishi wa BBC Jon Donnison, katika mji mkuu wa Libya,Tripoli,ameelezwa na afisa mmoja kutoka magharibi anayefahamu vyema kuhusu kesi hiyo kuwa makubaliano hayo yako ukingoni kukamilishwa. Lakini afisa huyo ameonya kuwa inaweza kuchukua miezi kadhaa kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa. Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Luis Moreno Ocampo atazuruLibyawiki hii. 

 Makundi ya kutetea haki za binadamu yamesema kuwa mfumo wa sheria nchini Libya hauna uwezo wa kushughulikia kesi yenye hadhi kama hii. Saif al-Islam, mwenye umri wa miaka 39, kwa sasa anashikiliwa na kundi la wapiganaji katika jimbo la Zintan la Libya.  

Alitatarajiwa kuchukua nafasi ya baba yake, marehemu Kanali Muammar Gaddafi. Haijajulikana ni lini kundi hili litamkabidhi kwa serikali ya Libya. Akihukumiwa Libya, Bw Gaddafi anaweza kukabiliwa na hukumu ya kifo.
Chanzo - BBC

Post a Comment

 
Top