Menu
 

Rais wa muda huko Mali ameapishwa Alkhamisi na hivyo kurejesha utawala wa kikatiba nchini humo baada ya wiki tatu za utawala wa kijeshi uliomtimua madarakani rais aliyekuwa amechaguliwa kwa njia ya demokrasia.

Dioncounda Traore ambaye ni spika wa bunge la nchi hiyo atashikilia nafasi ya urais wa Mali kwa muda wa siku 40 kwa mujibu wa katiba.

Akizungumza baada ya kuapishwa, Traore amewataka waasi wa Tuareg walioteka eneo lote la kaskaizni mwa nchi hiyo na kujitangazia uhuru kujiondoa kikamilifu katika eneo hilo la sivyo vita kamili vitaanzishwa dhidi yao. 

Dioncounda Traore amechukua madaraka baada ya Rais Amadou Toumani Toure aliyekuwa amepinduliwa na wanajeshi kuibuka kutoka mafichoni na kujiuzulu siku ya Jumapili.

Utawala wa kiraia umerejea Mali baada ya makubaliano kati ya wanajeshi waliokuwa wamenyakua madaraka na Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS.

Post a Comment

 
Top