Menu
 


Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Sindano ya ganzi yamsababishia mauti mtoto Tumaini Rataniel Mtajiha (5), mkazi wa Kijiji cha Hagomba Kata ya Itaka baada ya kuchomwa na daktari wa zahanati binafsi ya Sisika, inayomilikiwa na mwalimu mmoja katika Mtaa wa Ichenjezya, Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea Aprili 22 mwaka huu majira ya saa tano asubuhi baada ya mtoto huyo kufikishwa katika Zahanati binafsi, akiwa na jipu katika makalio ndipo Daktari alipompokea na kumtoza shilingi 20,000 baba mzazi wa marehemu Bwana Rataniel Mtajiha (45), ili apewe huduma.

Sababu ya kuchomwa sindano ya ganzi ni kutokana na mtoto huyo kuonaonekana ni mwoga hivyo achomwe sindano hiyo, na baada ya kuchomwa mtoto huyo alifariki papo hapo.

Baada ya tukio hilo Bwana Mtajiha alitoa taarifa Kituo cha Polisi Vwawa, ambapo walifika na kumchukua Daktari huyo (Jina linahifadhiwa), mwili wa mtoto na jalada lake pamoja na  sampuli ya dawa alizotumia hadi kwenye Hospitali ya Wilaya ili kufanyiwa uchunguzi majira ya saa 10:00 jioni.

Aidha, baada ya kutafakari kwa kina Hospitali hiyo ya wilaya, walitoa taarifa mkoani na kuagiza mwili ufanyiwe uchunguzi Aprili 23 mwaka huu, baada ya jopo la mkoani kuwasili wilayani Mbozi ili kufanya uchunguzi wa kina.

Kaimu kamanda wa Polisi mkoani Mbeya hakuweza kupatikana kuthibitisha tukio hili, na hivi sasa Daktari wa Zahanati hiyo anashikiliwa na Kituo cha polisi Vwawa akisubiri uchunguzi kufanyika.

Wakati huo huo baba mzazi Bwana Mtajiha, amesema hakutegemea mwanae kufikwa na mauti kwani, muda wote alikuwa anacheza licha  ya kukabiliwa na jipu hilo.

Post a Comment

 
Top