Menu
 Habari na Greyson Salufu, Mbeya.
Watu watatu wamefikishwa mahakamani kwa wizi wa pikipiki nambari T 462 AKG, aina ya Honda 250 inayomilikiwa na mwandishi wa habari wa Kituo cha redio cha Bomba FM kilichopo mbeya, ambaye pia ni mmiliki wa Blogu ya Kamanga na Matukio, aitwaye Ezekiel Kamanga.

Watuhumiwa hao wamefikishwa katika mahakama ya mwanzo ya Mwanjelwa iliyopo jijini hapa, nakusomewa mashtaka na mwendesha mashtaka wa Serikali mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Ales Mkasela.

Mwendesha mashtaka amewataja watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na Edward Sigala(29) mkazi wa Kabwe jijini hapa, Meadi Tosi(30) mkazi wa Manyenga wilaya ya Mbarali na Adriano Agustino(33) mkazi wa Mbalizi wilaya ya Mbeya Vijijini.

Watuhumiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Januari 31 mwaka huu, majira ya saa tatu na dakika arobaini na tano usiku nje ya Kituo cha redio eneo la Block T, jijini Mbeya.

Hata hivyo pikipiki hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 2,500,000 iliuzwa Kijiji cha Manyenga, Wilaya ya Mbarali kwa thamani ya shilingi laki 5, ambapo watuhumiwa walipewa malipo ya awali ya shilingi laki mbili.

Kwa pamoja watuhumiwa walikana kutenda kosa hilo, hali iliyopelekea kesi kuahirishwa hadi Aprili 17 mwaka huu itakapoanza kusikilizwa.

Katika kufanikisha wizi huo pikipiki hiyo ilibadilishwa nambari za usajili kutoka nambari zake za awali T 462 AKG na kubandikwa nambari nyingine T 303 BVR, hivyo baada ya uchunguzi kufanyika pikipiki hiyo ilikamatwa Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa, Machi 27 mwaka huu na kurejeshwa Mkoani Mbeya.

Washtakiwa wote watatu wamerudishwa rumande mara baada ya kukosa udhamini, na pikipiki hiyo iliwasilishwa mahakamani hapo kama kielelezo kwa kesi namba 252/2012.


Post a Comment

 
Top