Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Watu wasiofahamika wamevunja mlango wa maabara katika Kituo Cha Afya mji mdogo wa Tunduma, Wilaya ya Momba, Mkoani Mbeya majira ya usiku wa manane, mwezi Aprili 6 mwaka huu .

Hayo yamethibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Bwana Gabriel Kimoro, ambaye amesema vifaa hivyo vilivyoibiwa ni pamoja na mashine ya kupimia CD 4, darubini mbili, kompyuta moja, mashine ya Oygen(oksijeni) na mashine inayoitwa GENE-Expert ambayo thamani yake haijaweza kufahamika mara moja.

Aidha Mkuu wa upelelezi mkoani hapa Bwana Elias Mwita, amekiri kutokea kwa wizi huo na kwamba hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusika na wizi huo na upelelezi unaendelea ili kuwabaini wahalifu wa tukio hilo.

Baadhi ya vifaa hivyo nyeti vilivyoibiwa vilitolewa na wadhamini na vilikuwa msaada mkubwa kwa mji huo na nchi jirani ya Zambia na kwamba ni pigo kubwa kwa sekta ya Afya, alibainisha diwani wa Kata ya Tunduma Mheshimiwa Frank Mwakajoka.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Bwana Kimoro amewataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi la Polisi ili kufanikisha upatikanaji wa vifaa hivyo muhimu, kwani vilisaidia kupunguza adha kwa wakazi wa Tunduma, ambao awali walikuwa wakilazimika kusafiri hadi Vwawa katika Hospitali ya Serikali kupata vipimo mbalimbali vikiwemo vya maradhi ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Kuhara.

Hata hivyo huduma za Afya katika kituo hicho zimesimama kutokana na ukosefu wa vifaa hivyo na baadhi ya wagonjwa na ndugu zao kushindwa la kufanya, huku wananchi wakilaani vikali kitendo hicho kwani kinarudisha nyuma maendeleo katika sekta ya afya katika Wilaya ya Momba.

Post a Comment

 
Top