Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga, Rungwe.
Mkazi wa Kijiji cha Mwela, Kata ya Kandete, Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya, Bwana Chepe Mwasandube (50) ameamriwa kula udongo uliotumiwa kufukia kaburi la marehemu Sion Mwajungwa (52) Aprili 28 mwaka huu.

Akiongea na mwandishi wetu Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Anania Mwakitenga, amesema kuwa Bwana Mwasandube alituhumiwa kuwa ndiye aliyesababisha kifo cha marehemu huyo kilichotokea Aprili 27 mwaka huu kijijini hapo.

Wanakijiji walifika hatua hiyo baada ya mtuhumiwa huyo kutoonekana masibani baada ya marehemu kufariki, ndipo walipoamua kumuita eneo la makaburi kisha kumuamuru kula udongo ulio juu ya kaburi hilo na baadae walimpa pombe kwa ajili ya kushushia udongo huo aliokula.

Baada ya kumaliza kufanya hivyo aliambiwa adhabu yake imekwisha na yupo huru na kumtaka asirudie tena kufanya vitendo vya kishirikina kama hivyo.

Aidha baadhi ya mashuhuda wamekiri kuwa Bwana Mwasandube amekuwa akijihusisha sana na suala la ushirikina na kudai kuwa ndiyo silaya yake kijijini hapo.

Adhabu hizi kwa watu wanaojihusisha na ushirikina zimekuwa ni nyingi na kali  kwa siku za hivi karibuni, ambapo wengine huchomwa moto na mwingine kuzikwa akiwa hai mwishoni mwa juma kutokana na kuhisiwa kumuua mpwa wake kwa imani za kishirikina.

Vitendo hivi vimelaaniwa vikali na Kiongozi wa Mchifu wa kabila la Kisafwa Bwana Roketi Mwanshinga, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Itenzi Jijini Mbeya Aprili 30 mwaka huu ambapo shule tatu za kata hiyo ziliahirisha masomo ili kupisha tambiko kwa lengo la kuwafichua wale wote wanaojihusisha na imani za kishirikina kutokana na kudumaza maendeleo ya wananchi kutokana na kuishi kwa hofu.

Hata hivyo mara kadhaa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Abbas Kandoro amewaonya wananchi kutojichukulia sheria mkononi kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Post a Comment

 
Top