Menu
 

MTOTO Imrani Mwerangi (3) ambaye alipelekwa nchini India kwa matibabu baada ya kudungwa sindano iliyomsababishia mtindio wa ubongo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam, bado amelazwa katika Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU) cha Hospitali ya Hyderabad, India.

Taarifa iliyotolewa jana na wazazi wa mtoto huyo kutoka nchini India, ilisema hali ya Imrani bado ni mbaya. 

Machi mwaka huu Imrani alipelekwa nchini India na Serikali baada ya kulazwa katika ICU ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tangu Julai 28, 2011.

“ Tangu kipindi hicho madaktari wamekuwa wakipigania kuokoa maisha yake lakini bado amelazwa katika ICU ya Hospitali ya Hyderabad,India,” ilisema taarifa hiyo. 

Taarifa hiyo ilisema madaktari wanaomhudumia wamesema mtoto huyo ataendelea kutegemea matibabu katika  maisha yake yote.

“ Asante Mungu kwa kuendelea kumpigania mtoto wetu Imrani, leo anatimiza miezi kumi tangu alazwe katika ICU za Muhimbili na hapa India,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ya wazazi ilisema maisha kwao yamekuwa yenye changamoto kubwa lakini jambo kubwa sasa ni kutanguliza maombi kwa Mungu.

Kwa mara ya kwanza mtoto huyo alifikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Julai 28, 2011 kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa nyama zilizokuwa puani ambapo alipokewa na kufunguliwa jalada IP.No.A586301.

Kesho yake Julai 29, 2011 mtoto huyo aliingizwa katika chumba cha upasuaji mdogo wa nyama za puani lakini kabla ya upasuaji huo alidungwa sindano ya usingizi ambayo ndiyo iliyomsababishia matatizo mtindio wa ubongo.


Habari na - Raymond Kaminyoge

Post a Comment

 
Top