Menu
 

Habari na Angelica Sullusi, Mbeya
Watanzania wametakiwa kutumia mawazo yao katika kufikiri juu ya uboreshaji wa raslimali walizonazo ili zisaidie kupunguza umasikini miongoni mwa watanzani waishio chini ya dola moja kwa siku.

Hayo yamesemwa hivi karibuni Jijini hapa na Mkurugenzi Msaidizi wa masoko ya nje kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Jackline Maleko wakati wa tathimini ya ziara yao ya kutembelea mipaka ya nchi iliyopo mkoani hapa.

Maleko amesema kuwa walitembelea mipaka ya Tunduma wilayani Mbozi unaopakana na nchi jirani ya Zambia na Kasumulu wilayani Kelya unaopakana na nchi ya Malawi kwa lengo la kuangalia usafirishaji wa bidhaa mbalimbali mipakani hapo.

Amesema kuwa Tanzania imejaaliwa kuwa na bandari ambayo inategemewa sana na nchi za jirani kwa ajili ya usafirishaji wa bidhaa zao lakini pia inaunganishwa na kila pande na nchi zinazoizunguka lakini tatizo kubwa ni ugumu uliopo katika upitaji mipakani.

Amesema kuwa wakati wakitembelea mipaka hiyo walishuhudia msululu mkubwa wa magari yaliyojipanga kwa takribani kilometa 21 kutoka katika kituo na pia wasafirishaji wakilazimika kusubiri kwa siku nne hadi nane wakisubiri taratibu zikamilike tayari kwa kuvuka upande wa pili.

Aidha,amesema kuwa wakati umefika kwa mamlaka zinazohusika kujipanga upya na kuimarisha sekta kwa kupunguza ukiritiba uliopo katika mipaka yetu na kuitumia zivuri kwa maslahi ya nchi katika kuinua uchumi kwa kuiletea nchi wawekezaji wengi kwa manufaa ya watanzania.

Amesema kuwa licha ya Tanzania kujulikana duniani kama kisiwa cha amani lakini kiashara iko nyuma sana ambapo inashika nafasi ya 127 kati ya nchi 158 duniani zinazojihusisha na biashara ambapo inatokana na kuwepo kwa ugumu wa usafirishaji wa bidhaa katika mipaka yetu hali inayowakatisha tama wawekezaji.

Aidha,alizikata mamlaka za serikali za mitaa na Mkoa kuhakikisha inatengeneza miundombinu ya barabara,kuwawezesha wafanyakazi mipakani kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya utendaji kazi ikiwa ni pamoja na kuwalipa malipo baada ya kazi.

Tahimini hiyo imefanyika katika ukumbi wa Hill View Jijini hapa ikiwashirikisha watumishi wa mamlaka zote zinazohusika mipakani kutoka Wilaya za mipakani mkoani hapa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa ufadhiri wa USAID COMPETE.

Post a Comment

 
Top