Menu
 

Na Kenneth Ngelesi, Mbeya
Mkuu wa wilaya ya Mbeya Dr Noman Sigalla amelitaka jeshi la polisi kuacha kutumia ubabe na kutopendelea baadhi ya watu wa kada fulani katika kutekeleza majukumu yao kwani kufanya hivyo huchangia watu kutokuwa na imani na jeshi hilo na baadaye kutokea vurugu.
 
Rai hiyo alitoa na Mkuu huyo mpya wa wilaya mbele ya kamati ya ulinzi na usalama  ya wilaya wakati akikabidhiwa ofisi hiyo na mtangulizi wake aliyestaafu Evansi Balama ambapo  shughuli za makabidhiano  zilifanyika siku ya jumatano katika ofisi za Mkuu wa wilaya zilizopo Mbeya mjini.
 
Dr. Sigalla amesema kuwa kutokana na uzoefu wake kwamba baadhi ya askari wa jeshi hilo wamekuwa na tabia ya kutoa maamuzi yenye upendeleo wa jamii au vyama fulani  hivyo kupekelea vurugu sisizo za lazima.

Amesema kuwa kutokana na wananchi wengi kuwa na uelewa wa hali juu wamekuwa wepesi wa kung’amua mambo juu ya utendaji wa baadhi ya askari na wananchi wengi kutokubaliana na maauzi hayo.

Ametaka wananchi wa wilaya ya Mbeya kutokuwa tayari kunyanyasika na mtu kutokana na ubaguzi wa chama, kabila, kwani kwa kufanya hivyo ni kudhorotesha maendeleo ya wilaya na mkoa na taifa pia.

Amesema inapotokea mtu amevunja sheria za nchi jambo ambalo alisema kuwa hata kuwa tayari kuona mwanachi yeyote ananyanyasika na jeshi hilo kwa tatizo la kihitikadi za vyama.

Akizungumzia suala la migororo ya ardhi alisema kuwa anatambua wazi kuwa ni moja ya changamoto kwake kwani wilaya aliyotoka ya Hai Mkoani Kilimanjaro ndiko kwenye migogoro zaidi.

Mkuu huyo wa wa wilaya alisema hatalifumbia mambo jambo la watumishi wasio waaminifu katika ofisi yake kwani katika taarifa aliyopata kutoka kwa mtangulizi wake inaonyesha kuwa watumishi wengi wamekuwa wakitoa taarifa zisizosahihi hasa wakurugenzi.

Hata hivyo alitoa wito kwa watumishi wa serikali kufanya kazi kwa kushirikiana na vyombo vya habari kwani watumishi wengi wamekuwa wakikwepa kufanyakazi na wanahabari.
 
‘Inasikitisha sana na mara nyingine serikali inalaumiwa na wananchi kwa sababu ya watumishi ambao hawako  tayari kufanyakazi na vyombo vyetu vya habari, sasa unakuta kuna mradi serikali imetumia zaidi mil 800 lakini siku ya kufungua mnashindwa kuwaita waandishi wa habari ambao hata malipo yao hayazidi shilingi laki mbili  kama mnafanya hivyo mnadhani wananchi watajuaje kwamba serikali  yao inafanyakazi’ alisema Dr Sigalla

Kwa upande wake Mkuu aliyemaliza muda wake wa utumishi Evans Balama alisema wilaya ya Mbeya mjini ni ngumu kuliko wilaya zote alizowahi kufanyakazi hasa katika utekezaji wa majukumu ya kiserikali wananchi wengi wamekuwa wabishi.

Aidha amebainisha baadhi ya idara zenye matatizo na kumtaka Dr Sigalla kuwa makini nazo na zimekuwa zikileta migogoro mingi ikiwa ni pamoja na Idara ya Ardhi ambayo  watumishi wake wengi siyo waaminifu na Jeshi la polisi.

Dr Sigalla ameteuliwa kuwa  Mkuu wa wilaya ya Mbeya hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete akitokea wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro uteuzi ulifanyika nchi nzima, na kuapishwa Mei 16 pamoja na wakuu wote wa wilaya nane za mkoa na Mkuu wa Mkoa huyo Abasi Kandoro, Ikulu ndogo iliyopo Mbeya mjini na kukabidhiwa jukuma la kuziongoza halmashauri mbili ambazo ni Mbeya mjini na Mbeya vijijini.

Post a Comment

 
Top