Menu
 

Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Mbeya (CCM) Dk. Mary Mwanjelwa.
 ******
Na, Mwandishi wetu, Mbeya
MBUNGE wa viti maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya Dr.Mary Mwanjelwa amekanusha uvumi ulioripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa anatarajia kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Akitoa ufafanuzi katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya leo subuhi uliopo Sokomatola Jijini hapa, Mwanjelwa amesema habari hizo hazina ukweli wowote na hatarajii kufanya hivyo.

Alisema taarifa hizo ni uzushi na uongo kwa sababu yeye ni kada wa CCM wa siku nyingi ambaye amepewa dhamana na chama hicho kugombea ubunge kupitia jumuiya ya wanawake hivyo hatarajii kuwageuka kwa sababu bado anayo dhamana ya kuendelea kuwa Mbunge.

"Hizi taarifa ni uzushi mimi sijawahi kufikiria kuhama wala kufanya kinyume na matarajio ya chama changu kwa sababu mimi ni kada wa muda mrefu na nimechaguliwa na wananchi ili niwatumikie nikiwa ndani ya CCM hivyo nasikitika kuona nachafuliwa mimi na taarifa hizi zipo kwa wabunge wote wanasemwa sasa kwanini mimi nitolewe kafara na wengine waachwe" alilalama Mbunge huyo.

Awali waandishi walimuuliza kuwa kama amewahi kukaa na mwandishi huyo kuongelea hayo yaliyoandikwa au yamepikwa, Mwanjelwa alishindwa kujibu hali ambayo ilileta sintofahamu kwa wanahabari hao ambapo ilimlazimu kukaa zaidi ya dakika kumi akitafakari jibu sahihi huku akisaidiwa na Katibu wa chama hicho wa Mkoa wa Mbeya Verena Shumbusho.

Hata hivyo alikubali kuwepo kwa mazungumzo hayo baina yake na mwandishi wa habari hizo ambapo alisema hawakuongelea maswala ya yeye kukihama chama hicho na kuongeza kuwa amesingiziwa walichoongelea ni maswala ya wananchi kuhusu kutochaguliwa kwenye baraza la mawazirina si vinginevyo.

Taarifa za kukihama Chama cha Mapinduzi ambazo Mbunge huyo alikuwa akikanusha zilisema kuwa inatokana na ushawishi wa baadhi ya Viongozi wa Chadema mkoani Mbeya na Taifa baada ya uteuzi wa baraza jipya la Mawaziri uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa juma huku akishindwa kuwateua wabunge wa kuchaguliwa akiwemo Mwanjelwa badala yake kuteua wabunge wapya na kuwapa nafasi za uwaziri.

Katika hatua nyingine, Mwanjelwa alisema hawezi kuingilia mamlaka ya Rais na kwamba hakwenda Bungeni ili ateuliwe kuwa waziri bali yupo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wa mkoa wa Mbeya waliomchagua.

"Mimi siwezi kulalamikia kutoteuliwa kuwa waziri kama alivyoandika huyu mwandishi kwa sababu hayo ni mamlaka ya Rais ambayo mimi siwezi kuingilia hata hivyo sikwenda bungeni ili nichaguliwe kuwa waziri" alisisitiza Mwanjelwa.
Kwa hisani ya Kalulunga Blog.

Post a Comment

 
Top