Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoani Mbeya imeitelekeza Shule ya Sekondari Galijembe yenye Kidato cha tano na sita, iliyopo Kata ya Tembela wilayani humo.

Hayo yamebainishwa na wananchi baada ya mtandao huu kutembelea shule hiyo na kukuta vyumba vya madarasa yapatayo nane yaliyojengwa kwa nguvu zao, ambapo Serikali haijatoa chochote katika ujenzi huo wa shule hiyo.

Katika uchunguzi huo imebainika kuwa ni zaidi ya miaka 7 halmashauri imeitelekeza shule hiyo ya kisasa iliyojengwa kwa matofali ya saruji, kuezekwa kwa mabati na vyoo vya kisasa, kwa madai kuwa inaichukua shule hiyo kutoka mikononi kwa wananchi hao kwa lengo ya kuiendeleza.

Mtandao huu ulifanikiwa kuiona barua iliyoandikwa na uongozi wa kijiji hicho Mei 5, 2011 juu ya kumkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya vijijini, yenye Kumbukumbu nambari KIJ/145 yenye kichwa cha barua "KIJIJI CHA GARIJEMBE KUKABIDHI MAJENGO MATATU YENYE VYUMBA 8 VYA MADARASA KWA HALMASHAURI YA WILAYA YA MBEYA".

Aidha nakala ya barua hiyo ilipelekwa kwa Afisa mtendaji wa Kata ya Tembela na Diwani wa kata hiyo, Katibu tarafa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya, Ofisi ya Mbunge Jimbo la Mbeya Vijijini, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya na Afisa Elimu Sekondari.

Katika hali ya kushangaza au kusikitisha uongozi wa wilaya haujawahi kufika tangu kupokea kwa barua hiyo na wala hawajaiendeleza huku majengo kubaki kama maghofu, bila kujali pesa nyingi zilizowekezwa na wananchi wa kijiji hicho.

Hata hivyo barua hiyo ilisainiwa na Mwenyekiti wa Kijiji hicho kwa niaba ya kijiji, na kupokelewa na Halmashauri hiyo Mei 9, 201.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini Mchungaji Lackson Mwanjale, aliahidi kukutana na wananchi Mei 22 mwaka huu kwa nia ya kuzungumza naye, lakini licha ya kufika kijijini hapo kiongozi huyo alitoa sababu ya kuwahi msibani, hali iliyowasononesha wananchi hao wasijue la kufanya.

Kata hiyo ya Tembela ipo kilomita 22 kutoka jijini Mbeya na haina shule yoyote ya kidato cha 5 na 6, hivyo wanafunzi wanaojaliwa kuendelea na masomo hulazimika kusoma jijini hapa au Wilaya ya Rungwe ambako kuna shule hizo na kupingana na dhana ya kusogeza huduma kwa wananchi kuwa tete.

Shule hiyo imegharimu zaidi ya shilingi 80,000,000 ambazo zote ni nguvu za wananchi huku Serikali haijatoa chochote kama ilivyoada kuwa wananchi wajenge hadi kufikia usawa wa lenta na Serikali kumalizia.

Post a Comment

 
Top