Menu
 


Kamati ya Baraza la Wawakilishi inayochunguza ubadhirifu wa mali za Serikali ya Zanzibar imeitaka serikali kurejesha kiwanja alichopewa kinyume na sheria, mke wa Rais wa kwanza wa Zanzibar Mama Fatma Karume. Kwa mujibu wa ripoti ya  uchunguzi kiwanja hicho namba 186 chenye mita za mraba 750 kipo katika mtaa wa Kinazini, mkabla na Jemgo la historia la Dk. David Livingstone, mjini Unguja.

Ripoti imeeleza kwamba kiwanja hicho kilikuwa kikimilikiwa na Wizara ya Kilimo na Maliasili kabla ya kupewa Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) kujenga makao makuu yake. Uchunguzi wa kamati umebaini kuwa ZRB baada ya kupewa uwanja huo walishindwa kuuendeleza baada ya kupata uwanja mwingine katika eneo la Mazizini na kujenga makao makuu yake na uwanja ulirejeshwa Wizara ya Ardhi.

Ripoti imesema Wizara ya Kilimo ilitoa kiwanja hicho kwa ZRB kupitia barua ya Agosti 28, 2002 yenye kumbukumbu WKMMU/29/5/41/72 kwenda Wizara ya Ardhi ya kuwapa ZRB. Uamuzi wa Wizara ya Kilimo na Maliasili ulikubaliwa na Wizara ya Ardhi  na kukabidhi uwanja  kwa ZRB Septemba 9, 2002 kupitia barua yenye kumbukumbu namba MUNA/34/14/378/ VOl.1 na kutoa shahada ya haki ya matumizi ya ardhi ya Aprili 4, 2003.

Hata hivyo, ripoti imesema baada ya ZRB kupata sehemu nyingine ya kuendelea na ujenzi waliamua kukirejesha kiwanja hicho serikalini ambapo aliyekuwa Waziri wa  Ardhi, Makazi,Maji na Nishati, Mansour Yussuf  Himid, aliamua kiwanja hicho kumpatia mama yake Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, mwaka 2010.

Akihojiwa na kamati hiyo Desemba 7, mwaka jana, Waziri Mansour, ambaye sasa ni Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum alikiri  kiwanja hicho kumpa mama Fatma Karume baada ya kumuomba ili aweze kukitumia kwa shughuli zake za biashara ambazo hazijaelezwa.

 Hata hivyo, kamati imesema baada ya Waziri Mansour kuhojiwa juu ya kukosekana kwa maombi ya wahusika, alisema yalikuwepo maombi ya kampuni ya F&K Enterpreses LTD  katika faili maalum na alishangazwa na taarifa za kutoweka kwa nyaraka hizo.
Ripoti imeeleza kwamba baada ya mama Fatma kupewa uwanja huo ndani ya mwezi mmoja aliuuza kwa Kampuni ya F & K Enterprises Limited, ambapo anamiliki na hisa. Uchunguzi umebaini kuwa baada ya mama Fatma na wenzake kupitia kampuni hiyo kukabidhiwa uwanja huo waliuuza kwa Sh. milioni 150 kwa mfanyabiashara maarufu wa Zanzibar, Ali Shahib Khamis, na Waziri kumpatia hati miliki namba L.O.NO Z-53/S.178/2010/186 na R.O.NO Z-150/2010 ikiwa ni shahada ya matumizi ya ardhi iliyotolewa kwa mujibu wa sheria namba 12 ya ya ardhi ya mwaka 1992.

Akihojiwa na kamati juu ya kuuza ardhi hiyo ndani ya mwezi mmoja tangu kupewa mama Fatma, Mansour alisema hii ilitokana na kampuni yao kushindwa kufikia malengo waliojiwekea na hivyo kumua kukiuza kiwanja. Kamati imesema haikuridhishwa na utaratibu wa kisheria uliotumika kutoa kiwanja cha serikali baada ya mama Fatma Karume na wenzake kushindwa kuwasilisha nyaraka za kuthibitisha maombi yao kwa wizara kabla ya kutolewa kiwanja hicho.

“Mpaka tunatoa taarifa hii hakuna ushahidi wowote ambao mama Fatma aliuwasilisha pamoja na kuahidi angefanya hivyo kama alivyotakiwa kufanyaharaka iwezekanovyo,” ripoti imesisistiza.  Ripoti  imeeleza kwamba kamati ilichukua hatua mbali mbali za kufuatilia suala hilo ikiwa pamoja na kuwahoji watendaji wakuu wa wizara,  lakini imeshindwa kupata ushahidi wa maombi ya barua ya mama Fatma Karume au kampuni hiyo.

“Kamati kwa kauli moja inathibitisha kwamba hakuna ushahidi wa kuombwa kiwanja hicho na hivyo, ina wasiwasi waziri ametumia vibaya madarakan yake, ameamua kukimilikisha kiwanja cha serikali kwa mtu bila ya maombi yoyote kinyume na taratibu na sheria,” ripoti inasema.
Habari na - MWINYI SADALLAH
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

 
Top