Menu
 

Habari na Rashid Mkwinda, Ileje.
Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Ileje wamepiga kura za kutokuwa na imani na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo  Bi. Sylivia Siriwa kwa madai ya kuhusika na hujuma na ubadhirifu wa mali za halmashauri hiyo.

Hatua hiyo imefuatia tuhuma zilizoelekezwa kwake katika kikao cha baraza la Madiwani kilichoketi kujadili jaribio la wizi wa fedha za halmashauri zilizofanywa na watumishi wanne ambapo Mkurugenzi huyo alishindwa kuwachukulia hatua za kisheria.

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ileje Bw. Mohamed Mwala amesema kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya Baraza kujigeuza kamati ambapo Mkurugenzi alionekana kuhusika na makosa kwa kuwakumbatia watendaji hali ambayo imesababisha kutokuwa na imani naye
.
Amesema madiwani 22 waliohudhuria kikao hicho kati ya madiwani 25 wamepiga kura na kutia saini kuitisha mkutano maalumu ili kumwajibisha mbele ya mkuu wa mkoa. 

Miongoni mwa tuhuma anazokabiliwa Mkurugenzi huyo ni pamoja na kuipandikizia deni kiasi cha sh. bilioni 1.1 ambazo ni hewa halmashauri badala ya sh. milioni 251 ambapo pia Mkurugenzi huyo amekuwa hashirikiani na Mwenyekiti wala madiwani katika majukumu ya kila siku juu ya maendeleo ya halmashauri.

Kufuatia tuhuma hizo madiwani wamemuandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na nakala yake kupelekwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Ileje Katibu wa CCM wilaya na Katibu Tawala wa wilaya ambapo wametaka kuitishwa kwa kikao hicho ndani ya siku 21 kwa nia ya kuelezea tuhuma zake mbele ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya.

Post a Comment

 
Top