Menu
 

Mke wa Mwenyekiti wa Kijiji wa Kijiji cha Motomoto Bi Salome Ipopo aliyeketi, ikiwa amekwepa kamera, ambaye alivuruga mkutano kwa kuporomosha matusi kwa kila mwananchi aliyekuwa akichangia hoja katika mkutano wa hadhara baada ya mumewe kutuhumiwa kuuza ardhi ya kijiji na kufuja pesa za mradi wa maji.(Picha na Ezekiel Kamanga).
*****
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mke wa Mwenyekiti wa Kijiji wa Kijiji cha Motomoto Bi Salome Ipopo amevuruga mkutano kwa kuporomosha matusi jana kwa kila mwananchi aliyekuwa akichangia hoja katika mkutano wa hadhara baada ya mumewe kutuhumiwa kuuza ardhi ya kijiji na kufuja pesa za mradi wa maji.

Hayo yamebainishwa katika mkutano huo uliofanyika katika kijiji hicho ambapo kila aliyesimama kuchangia hoja mwanamke huyo alikuwa akimtusi na kumzomea kwamba akitaka akalie yeye kiti hicho.

Pamoja na mtuhumiwa Bwana Kassim Mwagala ambaye ni Mwenyekiti wa kijiji hicho, pia wananchi wamekosa imani na Serikali ya kijiji ambapo wajumbe wake ni Moses Njenge, Bi Tukuswiga Kyagi, Bwana Ally Sanga, Adrea Mwailafu, Erick Kipoke, Isaya Joel, Ezron Mwakajila.

Wengine ni Bi Betina Lwiba, Siasa Sagupina, Afyusisye Mwakalinga, Fredy Mwabutenga, Kulwa Mustafa na Mandela Ambwene na Afisa Mtendaji wa Kijiji Bwana Emmanuel Gwimile.

Katika mkutano huo Mwenyekiti na Halmashauri yake wanatuhumiwa kuuza hekari 8 kwa shilingi 250,000 tu hali inayoonesha ni ubadhilifu kwani hakuna kamati yoyote iliyokaa na kuidhinisha uuzwaji wa ardhi na kwenye mikutano iliyopita kiongozi huo alidai atazirejesha lakini mpaka sasa hajazirejesha.

Aidha alidai kuwa alipewa baraka na mkutano wa hadhara, kwani alidai fedha hizo zilitumika katika ukarabati wa Ofisi ya Serikali ya kijiji hali iliyopelekea wananchi kumzomea.

Uongozi huo pia unadaiwa kuchakachua pesa za mradi wa maji ambapo taarifa katika mkutano huo ilisomwa na Afisa mtendaji Bwana Gwimile, ambapo alidai kuwa makusanyo ya pesa za mradi huo ni shilingi 250,000 na kwamba zimetumiwa kwa ajili ya kufunga vifaa vya bomba kijijini hapo.

Agenda hiyo ilipingwa vikali na wananchi hao kwamba vyanzo vingine vya mradi huo havija ainishwa katika taarifa ya Afisa mtendaji, pia wananchi walihoji kwanini hakutumiwa fundi bomba wa kijiji hicho Usaje Edson Mwambeje, ambaye amesomeshwa na kijiji kwa ajili ya kuendesha mradi huo.

Mbali ya taarifa hiyo kukataliwa pia wananchi walikataa kusomewa taarifa ya mapato na matumizi hadi mkutano utakapoitishwa tena..

Kwa upande wake fundi huyo amesema kwamba hakupewa ushirikiano wa kutosha na Kamati nzima ya maji kijijini hapo na kwamba aliitwa na Mwenyeki wa kijiji akiwa na mke wake ofisini, wakimtaka asiendelee na kazi hiyo na hivyo kamati hiyo kuiongoza mwenyewe, ambapo alitumia fursa hiyo kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kufuatia majibizano hayo wananchi hawakuridhishwa na majibu ya Mwenyekiti na kwamba agenda nyingine zilifichwa hali iliyosababisha wananchi kugoma kuendelea na mkutano na kiongozi huyo kuahirisha mkutano, huku wananchi wakimzomea na kumtaka yeye na serikali yake kujiuzuru mara moja, kitendo ambacho alikipinga na kudai kwamba agenda hizo ziletwe ili mkutano uitishwe siku nyingine.

Hata hivyo kabla ya mkutano huo Afisa Mtendaji alimzuia Bi Tupokigwe Ipopo, asiulize swali akidai kwamba si mkazi wa kijiji hicho, na wananchi kumzoea kiongozi huyo na kudai kuwa mwanamke huyo ni mkazi halali na ana haki ya kuuliza swali lolote.

Wakati huo huo Wakazi wa Kijiji cha Malamba, wilayani humo wamemtaka Mwenyekiti wao Ngumbushe Mwalyego  kurejesha, pesa za kijiji hicho shilingi 1,400,000 ambazo alizipokea baada ya tozo la faini ya mifugo kutoka kwa wafugaji wa kisukuma, ambapo alikiri kupokea pesa hizo na kwamba angezirejesha lakini tangu Novemba mwaka jana hajaziresha na hataki kuitisha mikutano.

Wameongeza kuwa endapo hatafanya hivyo watamuondosha madarakani mara moja pamoja na serikali yake.

Post a Comment

 
Top