Menu
 

MKUU wa wilaya ya Mbozi Gabriel Kimolo ametangaza kujiudhuru wadhifa huo kutokana na sababu tatu alizozitaja kuwa kikwazo kikubwa katika utendaji kazi wake.
 Kimolo alitangaza uamuzi huo Mei 4,2012 katika kikao chake na waandishi wa habari kilichofanyika katika hoteli ya Beaco iliyopo Forest mpya jijini Mbeya.

Alisema mpaka anzungumza na wanahabari alikuwa amekwishamwandikia barua rais kumweleza nia hiyo na nakala ya barua hiyo kuipeleka kwa mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro,ofisi ya waziri mkuu na ofisi ya waziri wa tawala za mikoa na serikali za mikoa(Tamisemi).

Akielezea sababu za kujiuzuru kwake alitaja sababu ya kwanza kuwa ni kutoteuliwa upya kwa wakuu wa wilaya tangu mkataba wao wa kazi ulipomalizika baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Alisema hatua hiyo imewasababishia kuendelea kufanya kazi pasipo mpango mkakati kwakuwa hawajui lolote linaloendele juu yao hivyo kujikuta wakiishia kufanya shughuli zao kwa zima moto.

Alisema kwa kufanya hivyo hakuweza kuwatumikia wananchi wa wilaya hiyo na kuona kama mtu asiyestahili kuendelea kuwa kiongozi wao huku akiongeza kuwa hali hiyo pia imemuathiri yeye na familia yake kwa kiasi kikubwa kwakuwa alilazimika kusimamisha mipango yake yote.

Kimolo aliitaja sababu ya pili iliyopelekea uamuzi huo kuwa ni ukumbatiaji wa vitendo vya kifisadi kunakofanywa na baadhi ya viongozi wa serikali ambao umekuwa tatizo kubwa katika utendaji kazi wake.

“Sababu hii inatokana na hali halisi iliyopo wilayani Mbozi juu ya biashara ya kahawa mbichi ambapo licha serikali ya wilaya na mkoa kuweka msimamo wa kutoruhusu ununuzi wa kahawa mbichi inaonekana wizara bado inatoa vibali vya ununuzi huo bila kujali kuwa wananchi wanaumia” alisema

Alisema suluhisho la mgogoro wa ununuzi wa kahawa mbichi limeendelea kuwa kitendawili kwakuwa licha ya viongozi wa wizara waziri Profesa Jumanne Maghembe na naibu wake Christopher Chiza kufika wilayani hapo bado walikuwa na majibu yasiyoridhisha na kuonesha dhahiri kuwa maamuzi ya wilaya na mkoa hawaridhiki nayo.

“Ni dhahiri kuwa uongozi wa wizara ndiyo unayoyapa makampuni kiburi cha kuendelea kuwaumiza wananchi kwa kuwaibia kupitia ununuzi wa kahawa yao mbichi na waoa kupata faida kubwa mno.Ni kutokana na kinga hiyo wenye makampuni wanafikia hatua ya kututukana wakisema hawazungumzi na mbwa bali mfuga mbwa” aliongeza.

Aliitaja sababu ya tatu kuwa ni hali ya wizi na ucheleweshaji wa pembejeo za ruzuku zinazotolewa na serikali kwaajili ya kuwasaidia wakulima wadogo ambapo kwa wilaya yake malalamiko yamekuwa makubwa hali inayowashushia hadhi viongozi wa halmashauri na wilaya kwa uozo uliofanywa na uongozi wa wizara.

Post a Comment

 
Top