Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga.
Moto mkubwa umezuka na kuteketeza Bar ya Tukuyu iliyopo Mtaa wa Utukuyu, Kata ya Uyole Jijini Mbeya, na kuteketeza kila kitu kilichokuwemo ndani ikiwa ni pamoja na vinywaji na samani.

Bar hiyo inayomilikiwa na Bwana Timoth Mwampashi, ambaye alipangisha katika nyumba inayomilikiwa na Bwana Kipenula Kyando na imedaiwa kuwa moto huo umetokana hitilafu ya umeme iliyotokea majira ya 6:45 usiku Mei 13 mwaka huu kwa mujibu wa mhudumu wa bar hiyo Lyego Miston (24) na Meneja wake Bwana Erick Jairos (24).

Naye, Afisa mtendaji wa mtaa huyo Bwana Chesco Anthon Lumato amesema baada ya kupata taarifa za moto huo alitoa taarifa kwa Diwani wa Kata hiyo Bwana Kambi Ngela Mwasoni, ambaye alitoa taarifa kikosi cha Zimamoto ambapo walifika saa 6:55 usiku na kufanikiwa kuzima moto huo.

Kama moto huo usingedhibitiwa mapema ungeweza kuteketeza maduka zaidi ya 11 yaliyoizunguka Bar hiyo.

Kwa upande wake shuhuda wa tukio hilo Bwana Gervas Haule alilipongeza shirika la Umeme mkoani Mbeya kwa kufika mapema na kukata umeme ili usilete madhara katika nyumba nyingine.

Hata hivyo Diwani huyo Mheshimiwa Ngela amewashukuru wananchi kwa moyo wao uzalendo katika kusaidia uokoaji wa baadhi ya vitu ingawa baadhi waliiba viti 6 vya Bar hiyo.

Post a Comment

 
Top