Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Shona Giba mwenye umri wa mwaka mmoja amefariki dunia kwa kukatwa na panga kichwani  baada ya mtu au watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kuvamia nyumba ya wazazi wake Kijiji cha Mamba, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Tukio hilo limetokea majira ya saa 7 usiku Aprili 16 mwaka huu, baada ya watu hao kuvamia nyumba kwa kuvunja malango kwa kutumia shoka kisha kuingia ndani ya nyumba ya Bwana Giba Mawe (30) na kumjeruhi mguu wa kulia kwa panga huku wakimjeruhi mkewe Bi Pilika Kabese (25), ambaye naye alijeruhiwa kichwani na mguu wa kulia.

Marehemu alifariki papohapo na majambazi hayo yalipora pesa taslimu shilingi 7,540,000 na kutokomea nazo kusikojulikana.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa Advocate Nyombi amesema Jeshi la polisi linamshikilia Bwana Ndangu Mbeshi (35) ambaye ni mkulima na mkazi wa Chunya na upelelezi wa tukio hili unaendelea.

Wakati huohuo ameongeza kuwa moto mkubwa umezuka majira ya saa 1:30 jioni Mei 15 mwaka huu katika Shule ya Sekondari Chimala Mission iliyopo Wilaya ya Mbarali na kuteketeza kabisa bweni la wasichana na kila kitu kilichokuwemo, nguo, vitabu na samani.

Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na juhudi za wananchi zilifanikisha kuzima moto huo na thamani mali zilizoteketea haijaweza kufahamika mpaka sasa.

Aidha Kamanda Nyombi amesema kuwa majira ya saa 12:30 jioni huko eneo la Utengule, Wilaya ya Mbeya Vijijini Polisi wakiwa doria waliwakamata watu wawili Mwanzuka (19) na Dan Joseph (20), wakiwa na kete 99 za bangi sawa na gramu 480.

Mbinu iliyotumika ni kuficha bangi hiyo katika mfuko wa rambo na watuhumiwa ni wavutaji na wauzaji wa bangi na kwamba watuhumiwa wapo mahabusu na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani ili kujibu shtaka linalowakabili..

Post a Comment

 
Top