Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Raia 6 wa nchi ya Somalia wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kisha kupinduka katika Kijiji cha Luswiswi, Wilaya ya Kyela, Mkoani Mbeya.

Tukio hilo limetokea mei 7 mwaka huu majira ya saa nne usiku ambapo gari lenye nambari T 934 AAR aina ya Fuso linalomilikiwa na Msuya mkazi wa Arusha lililokuwa na wasomalia hao ambayo idadi yake haijafahamika walipokuwa wakipita njia za panya kwa nia ya kwenda nchi ya Malawi kupitia wilaya ya Ileje.

Dereva wa gari hilo hakuweza kupatikana baada ya kutoroka mara baada ya ajali hiyo kutokea na kwamba lori hilo lilikuwa katika mwendokasi dereva huyo alishindwa kulimudu katika kona hali iliyopelekea gari kupinduka na kuingia korongoni.

Baada ya ajali hiyo waliojeruhiwa walijikongoja mpaka barabarani na wanakijiji wa kijiji cha Luswiswi kutoa msaada wa hali na mali ambapo walitoa taarifa kwa Afisa mtendaji wa kijiji Bwana Eliki Kibona.

Bwana Kibona alitoa taarifa kwa Halmashauri ya wilaya na Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Ileje ambapo walituma gari kwa ajili ya kuwachukua majeruhi wapatao tisa ambao wamelazwa katika Hospitali ya wilaya hiyo iliyopo Itumba Ileje.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ileje Mheshimiwa Aliko Kibona alifika eneo la tukio na kuwashukuru wananchi wa kijiji hicho kwa moyo wa upendo wa huruma kwa ajili ya kutoa msaada wa hali na mali.

Miili ya raia hao wa Somalia imehifadhiwa katika hospitali hiyo, huku jeshi la polisi likifanya uchunguzi wa tukio hilo.

Aidha Idara ya uhamiaji mkoani hapa ilituma maafisa wake eneo la tukio ili kubaini uhalali wa kuwepo nchini wasomali hao.

Hata hivyo Kaimu Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani hapa Barakiel Masaki, amethibitisha kupata taarifa kuhusiana na tukio hilo na kwamba amemtuma Afisa wake na kwamba atatoa taarifa mara baada ya kurejea.

Wimbi la raia wa Ethiopia na Somalia kupitia nchini kwa njia haramu limezidi kukua huku baadhi ya wananchi kushindwa kutoa taarifa kwa idara ya uhamiaji na Polisi.

Post a Comment

 
Top